Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) limesikitishwa kuendelea kushikiliwa kwa Mratibu wa Uhamasishaji Bavicha Taifa Ndugu Twaha Mwaipaya na Jeshi la Polisi. Twaha Mwaipaya alikamatwa Juni 30, 2022 na Jeshi la Polisi Morogoro mjini, ambao kesho yake ya Julai Mosi, 2022 walidai kuwa amesafirishwa kwenda Dodoma. Julai Mosi, 2022 na Julai 02, 2022 viongozi wa chama waliopo Dodoma walizunguka vituo vyote vya polisi bila mafanikio. Leo ni si siku ya tatu tangu kukamatwa kwa Ndugu Twaha Mwaipaya.

Jana Julai 02, 2022 saa sita mchana Jeshi la Polisi likiwa na Twaha Mwaipaya walifika nyumbani kwake Kisewe Mbagala, Dar es salaam kufanya upekuzi. Baada ya upekuzi huo hawakuondoka na chochote, ila hawakuwa tayari kueleza wanamshikilia katika kituo gani.

Aidha, leo Julai 03, 2022 viongozi wa Bavicha Taifa wamezunguka vituo vyote vikubwa vya Polisi Dar es salaam na kuambiwa kuwa ndugu Twaha hayupo, isipokuwa kituo cha Polisi Mburahati. Viongozi hao walipofika Kituo cha Polisi Mburahati walijibiwa kuwa Ndugu Twaha Mwaipaya ametolewa asubuhi ya leo kituoni hapo kupelekwa Dodoma. Pia kuna taarifa kuwa Ndugu Twaha bado anashikiliwa katika kituo hicho cha Mburahati.

Jeshi la Polisi kuendelea kumshikilia Ndugu Twaha Mwaipaya kwa siku tatu bila kupewa dhamana au kupelekwa mahakamani ni kinyume cha sheria. Hivyo, Jeshi la Polisi limuachie huru au limpatie dhamana. Bavicha tunalitaka Jeshi la Polisi lijitokeze kueleza yuko mkoa gani na kituo gani cha polisi pamoja na kutoa nafasi kwa uongozi wa Chama, familia yake na mawakili kuweza kumuona kujua hali yake na kulinda haki zake.

Baraza limewasilisha taarifa hiyo kwa Chama na tayari Chama kimeelekeza mawakili kuanza maandalizi ya kuchukua hatua dhidi ya Jeshi la Polisi na Serikali kuwezesha Twaha Mwaipaya kuachiliwa huru au kupata dhamana na haki zake zingine kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria zinazohusika.

Imetolewa leo Julai 03, 2022

Apolinary Boniface
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano – Bavicha

Share Button