Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeo (Chadema), Mhe. Tundu Lissu, ameahidi kutompitisha mtu yeyote katika maumivu makali ya majeraha mithili ya yale aliyoyapitia yeye baada ya kunusurika shambulio lililolenga kukatisha uhai wake, Septemba 7, 2017, akiwa kwenye shughuli za Bunge, jijini Dodoma.

Mbali ya ahadi hiyo ambayo ameitoa mbele ya madhabahu ya Mungu, Mhe. Lissu ametumia fursa ya ibada hiyo, kuwashukuru Watanzania wote, wa dini na madhehebu mbalimbali kwa sala na maombi yao wakati alipokuwa katika wakati mgumu hospitalini, kuanzia jijini Dodoma, nchini Kenya na kisha Ubelgiji, akitibiwa baada ya shambulio hilo ambapo risasi zipatazo 16 zilimpata mwilini mwake.

Mhe. Lissu ameyasema hayo asubuhi ya leo, Jumatatu, Agosti 10, 2020, alipofanya ibada ya shukrani katika Kanisa la Mtakatifu Rita wa Kashia lililopo Ikungi, katika Jimbo la Singida Mashariki, mkoani Singida, iliyoongozwa na Paroko Laurent Bahaji wa Parokia ya Mtakatifu Rita wa Kashia.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania wote kwa dini zao kwa kuniombea wakati nilipokuwa mahututi, nilipopata nafuu mpaka nilipopona kabisa.

“Mungu wetu ni wa ajabu sana. Amesikia sala zenu na leo nipo nanyi mzima wa afya tayari kutekeleza kazi iliyosalia. Niliumizwa sana ndugu zangu. Wiki mbili za mwanzo baada ya kushambuliwa nilipata maumivu makali ambayo sikuwahi kuhadithiwa. Mwili ulikuwa unawaka moto. Naahidi sitampitisha mtu yeyote kwenye maumivu yale niliyoyapata hata kama atakuwa amenikosea kwa kiwango gani,” amesema Mhe. Lissu.

Mhe. Lissu aliambatana na Mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Salum Juma Mwalim.

Viongozi hao wawili, baada ya ibada hiyo, wameendelea na ziara ya kutafuta wadhamini 200 kutoka mikoa 10 ya Tanzania, ikiwa ni mojawapo ya masharti katika fomu za uteuzi wa kuwania nafasi hiyo ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya juzi kudhaminiwa na wananchi wa Mkoa wa Dodoma, leo watakuwa mkoani Singida katika eneo la Ikungi, Singida Mashariki na Ilongero, Singida Kaskazini.

Siku ya kesho Jumanne, Agosti 11, mwaka huu, watakuwa Igunga na Nzega, kwa ajili ya kupata wadhamini mkoani Tabora.

Imetolewa leo Jumatatu, Agosti 10, 2020 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Chadema

Share Button