MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI-, WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA KUSIMAMIA NA KUENDELEZA UVUVI WA BAHARI KUU WA MWAKA 2020 (THE DEEP SEA FISHERIES MANAGEMENT AND DEVELOPMENT ACT, 2020)

(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2016)

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, kwa heshimwa kubwa naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunipa nguvu na hivyo kuweza kusimama mbele ya ukumbi huu ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kiuhusiana na mapendekezo ya Serikali kuhusiana na muswada huu wa sheria ulio mbele ya Bunge letu.
  3. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitowashukuru watanzania wote, kwa kuendelea kuwa pamoja licha ya taharuki kubwa inayoendelea ya janga kubwa la ugonjwa wa Corona. Sambamba na hilo niwashukuru wanachadema kote walipo kwa msimamo wao usioyumba wa kuendelea kutuunga mkono katika kipindi hiki kigumu sana ambacho chama chetu kinapitia.
  4. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwa viongozi wetu wakuu wa chma kwa uvumilivu wao mkubwa kutokana na madhila wanayokutana nayo kutokana na msimamo wao wa kuhakikisha CHADEMA inaendelea kusimamia kile ambacho inaamini ni sahihi, kuna usemi unaosema kuwa; “The difference between the impossible and the possible lies in person’s determination”, hivyo basi ninaamini wana-CHADEMA na watanzania wote watafanya yale yasiyotarajiwa na washindani wetu hapo Oktoba.
  5. Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2020 pamoja na kuweka masharti bora ya usimamizi, udhibiti na uhifadhi wa rasilimali za uvuvi katika Ukanda Maalum wa Uchumi wa Bahari (EEZ). Kutungwa kwa Sheria hii kutaimarisha utekelezaji wa matakwa ya Sheria na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa katika kudhibiti na kuhifadhi rasilimali za uvuvi. Aidha, Muswada unaopendekezwa unakusudia kuifuta Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Sura ya 388.
  6. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kupitia muswada uliombele yetu.
  7. MAONI NA MAPENEKEZO YETU KATIKA MAPITIO YA MUSWADA
  8. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla maudhui ya muswada kwa mtazamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani yako vizuri, kwani mambo ambayo tumekuwa tukiyashauri kwa kipindi chote toka mwaka 2005 hadi sasa kwa kiwango kikubwa yamezingatiwa, tunaamini kuwa eneo hili la uvuvi wa bahari kuu kama litasimamiwa vizuri ni dhahiri hazina kubwa ya fedha za kigeni na ajira kwa watanzania walio wengi itapatikana bila ya matatizo yoyote.
  9. Mheshimiwa Spika, mambo ambayo tunaona yamezingatiwa na kupitiliza kiasi kwamba yanaweza kukimbiza hata wale ambao walikuwa na nia ya kuwekeza katika tasnia hii, ni muhimu yakafanyiwa marekebisho kabla ya sheria hii kuanza kutumika.
  10. Mheshimiwa Spika, kifungu cha (3) cha muswada kinachohusiana na tafsiri ya maneno yanayotumika katika muswada, kuna baadhi ya maneno yameshindwa kupatiwa tafsiri na badala yake inatolewa kwenye majukumu ya Mkurugenzi, mfano ni maneno “fishery inspector na fishery observer” hawa ni watu wawili tofauti je ni akina nani hasa? Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni muhimu sana katika kifungu hiki cha tafsiri kutoa maana inayoeleweka kwa wale wataokuwa wanatumia sheria hii ili kuondoa mkanganyiko usio kuwa na ulazima.
  11. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5(3) cha muswada kinachohusu makao makuu ya mamlaka kuwa yatakuwa ni Zanzibar, au mamlaka inaweza kufungua ofisi yake katika eneo lolote la Tanzania bara, au nje ya Tanzania Zanzibar-((3) The headquarters of the Authority shall be in Tanzania Zanzibar, ———- or outside Tanzania Zanzibar)
  12. Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uelewa uliokusudiwa ni vyema haya maneno “outside Tanzania Zanzibar” yakafutwa au kama ndio hivyo ilivyokusudiwa maana yake ni kuwa ofisi ya Mamlaka inaweza funguliwa hata Mombasa, Comoro, Ushelisheli nakadhali kwani kwa maneno hayo sheria itakuwa inatoa ruhusu kwa Mamlaka kufanya hivyo.
  13. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 6(3)(iii) cha muswada kuhusiana na kazi za mamlaka hii inayoundawa, kinachosema kwamba; “concluding agreements for fisheries access by non-citizens and non-nationals, including foreign fishing vessels”. Hapa ndipo kumekuwa na tatizo kubwa sana kwa kuwaachia watu ambao tumewapa mamlaka kwa kuwaamini lakini ukweli wanatuangssha sana. Mikataba hii kama ule miswada ya The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act na “the Natural Wealth and Resources (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act 2017 (“Contract Review Act”)”.  Sheria ambazo zilipitishwa na Bunge letu zinahusika vipi hapa katika kifungu hiki?
  14. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuacha majukumu makubwa kama haya kwa Mamlaka bila kuwepo na chombo kingine tofauti kuangalia jinsi mikataba hiyo ilivyo na masalahi au hasara kwa nchi ni shida sana. Aidha hoja yetu hii inaendana na kifungu cha 102(2) (b) “all licences, permits, authorizations and other instruments or documents granted or issued under the repealed Act, shall, so long as they on the date of commencement of this Act continue in full force and effect until they expire, cease to have effect or are replaced;”
  1. Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama haya, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa itakuwa vigumu kuweza kutimiza lengo la utunzi wa sheria hii. Tuna wasiwasi inaweza tokea tasnia moja ikawa inatumia sheria mbili tofauti kama ambavyo inatokea kwenye tasnia ya madini kwa baadhi ya makampuni kutumia sheria ya zamani na mengine kutumia sheria mpya kutokana na mikataba na leseni na vibali vilivyokuwa vimetolewa kabla ya matumizi ya sheria mpya. Jambo la kuangangalia ni kwamba uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu ni chombo cha mtu anayefanya biashara hiyo tu kuwa kina viwango vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria tu na sio jambo lingine. Hivyo ni tofauti sana na uwekezaji kwenye rasilimali zingine kama mafuta, gesi na madini mengine.
  2. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 15 kinachohusu uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, na kifungu kidogo cha (3) kinasema kuwa; “(3) For the purpose of ensuring equal representation of both sides of the Union, the Director General and Deputy Director General shall, at any given time, be appointed one from Mainland Tanzania and the other from Tanzania Zanzibar, and subsequent appointments for each position shall alternate between the two sides of the Union”.
  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kifungu hiki kinachoweka ulazima wa watu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa mazingira ya sasa ya Dunia kuhusu ajira ni dhahiri kifungu hiki haikileti maana sana. Tukumbuke kwamba Mamlaka inayoanzishwa ni chombo cha kibiashara na hivyo tuangalie mtu wa kuendesha chombo hiki kuwa ni mtu makini bila ya kuangalia uraia wake, kinachohitajika ni kuhakikisha anaendesha Mamlaka hii ili ikidhi matakwa ya uwepo wake.
  2. Mheshimiwa Spika, tunakumbusha tena katika taasisi kama hizi kuingiza siasa katika utendaji ni jambo ambalo litapelekea kushindwa kufikiwa kwa lengo kuu la uanzishwaji wake kabla hata kuanza kazi zake kwa mujibu wa sheria, hivyo basi tutafute watu makini ikiwezekana toka kwa wenzetu ambao wamefanya kazi hizi kwa muda mrefu sana na wanavyo viwanda vingi vya samaki (fish processing ports),tusitunge sheria ya ya kutufunga katika kupata watendaji wazuri wenye ujuzi na exposure kubwa katika kile tunachotaka kukifanya. Kwa kuweka kumbukumbu sawa ni kwamba Mtendaji Mkuu wa Kwanza wa TANROADS hakuwa Mtanzania, vivo hivyo kwa MSD, hivyo basi jambo hilo halitakuwa na ukakasi kwani kinachohitajika ni kuhakikisha mamlaka inafanya kazi kwa faida zaidi na mafanikio makubwa.
  3. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 18 cha muswada kinachosema kwamba; “A person authorized to perform the functions of the Authority shall not be personally liable for any loss or damage suffered to any person by reason of anything done or not done in good faith”. Kambi Rasmi ya Upinzani mara nyingi imekuwa ikikataa utunzi wa sheria zenye kifungu hiki kwani katika tafsiri ya maneno hakuna maana ya “good faith” na hiyo nia njema inaanzia wapi na kuishia wapi? Tukumbuke biashara hii inahusu sana sana bidhaa zinazowahi kuharibika-“Perishable products”, hivyo jambo lolote litakalofanywa na watendaji dhidi ya mfanyabiashara mwenye leseni na vibali halali kuhusu biashara yake, ni dhahiri jambo hilo ni hujuma dhidi yake na mhusika ni lazima awajibike katika hasara hiyo kwa mujibu wa sheria.
  4. Mheshimiwa Spika, dhana ya kifungu hiki inaendana na kifungu cha 67(7) ambacho kinasema Mkurugenzi Mkuu or wakaguzi au afisa yoyote wa mamlaka hatawajibika kwa uharibufu au kuoza au kupotea ubora wa bidhaa zilizo kamatwa.  Haki hapo iko wapi kwa mfanyabiashara?
  5. Mheshimiwa Spika, sasa ni kipindi cha matumizi ya teknolojia hivyo tusitunge sheria kwa kuangalia au kuzipa nyufa au kukinga makosa ambayo tayari yamefanywa huko nyuma na Serikali kuingia hasara kubwa kutokana na makosa hayo. Tutunge sheria kulingana na wakati uliopo na ujao ili tuokoe tasnia hii, na pia tusiweke kinga kuwa makosa au hujuma itafanyika hivyo iwekewe kinga.
  6. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 24(7) cha muswada kinasema Waziri ndiye atakaetunga kanuni kuhusiana na taratibu za utawala kama vile kuweka faini na adhabu na vile vile vibali. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri utaratibu huo hasa faini na adhabu viwe ndani ya sheria nasio kwenye kanuni kwani historia inaonesha kuwa wahusika wanakuwa na matumizi mabaya ya madaraka hayo, hivyo ni muhimu sana  mambo hayo yakawa ndani ya sheria mama.
  7. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 53(1), (2) na (3) vinahusu usiri wa taarifa, Kambi Rasmi ya Upinzani inajiuliza katika biashara inayohusu rasilimali za taifa, na tukumbuke kuwa biashara kubwa hapa ni uvuvi wa samaki na taarifa zote hapa kwa ufahamu wetu ni kuhusiana na uvuvi  wa samaki na mazao ya baharini wa kiasi gani kimevuliwa na wenye meli zilizosajiliwa, mapato ya nchi sio siri hivyo basi kwa kila mwenyekutaka kufahamu ni haki yake kufahamu. Je jambo hilo samaki au mazao mengine ya baharini ni kiasi gani yamepatikana nalo linatakiwa kuwa siri? Aidha, usiri ni ukiritimba na ukiritimba ndio chanzo kikuu cha rushwa kubwa kubwa hasa katika rasilimali zetu. Kwa muktadha huo tunataka vifungu hivi vya usiri wa taarifa vifutwe.
  8. Mheshimiwa Spika,kifungu cha 67(1) kuhusiana na uuzaji wa bidhaa zilizokamatwa na zinazoharibika kuwa Mkurugenzi mkuu atafanya mashauriano na Mkurugenzi wa Mashtaka kuwa ziuzwe au kutoa  idhini ya kuuza, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa Mamlaka sahihi kwa jambo hilo ni ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tukumbuke kuwa tasnia hii ya Uvuvi katika bahari kuu inahusu makampuni ya nje na ikitokea chochote katika mchakato wa kibiashara mhusika mkuu atakuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sio Mkurugenzi wa Mashtaka.
  9. Mheshimiwa Spika,kifungu cha 68 cha muswada kinahusu uachiwaji wa chombo na bidhaa baada ya kuwekwa kwa dhamana na mahitaji mengine. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kifungu hiki kinaweka mazingira makali, magumu na ya kukomoana sana na mbaya zaidi hakikusema pale chombo kilichokamatwa kabla ya kuachiwa kitakuwa kimesimama tu bila kufanya kazi yoyote na uangalizi wake utakuwaje? Wenzetu wa Botswana waliopokuwa wanakamata meli katika eneo lao la bahari kuu, meli hizo zinaendelea kufanyakazi na wahusika hao hao huku kesi inaendelea na nchi inaendelea kunufaika na sio kuiacha meli ikaoza na kuharibika.
  10. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 71 cha muswada kinachohusu kutaifishwa kwa chombo na bidhaa zilizomo kwenye chombo wakati kinakamatwa, lakini muswada unasema mali zote zilizotaifishwa zitakuwa na mali za Serikali, vivo hivyo na kwa kifungu cha 72. Kambi Rasmi ya Upinzani inakumbusha ukamataji wa meli ya wavietnam maarufu kama meli ya Samaki wa Magufuli, meli hiyo ilishindwa kufanya kazi na badala yake ikahujumiwa na mwisho Serikali ikatakiwa kulipa gharama za meli na bidhaa zilizokuwemo baada ya kesi kumalizika. Hivyo basi badala ya kusema itakuwa ni mali ya Serikali muswada uende mbele zaidi kueleza ni eneo gani meli au mali hizo zitakapowekwa ili kuondoa mivutano na ukiritimba usiokuwa na maana unaokuwa na lengo la hujuma au maslahi binafsi.
  11. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 86 cha muswada kinatoa uwezo kwa Mamlaka kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha pale inapopata idhini kutoka kwenye Kamati Tendaji, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa Mamlaka inatoa mpango wa matumizi ya fedha za kukopa, lakini kifungu hakioneshi njia au mpango gani wa kurejesha mkopo huo. Taasisi nyingi zinashindwa kuaminika kutokana na kutokuwa na mpango imara wa kurejesha mikopo na mwisho wa siku hiyo “burden” ya mkopo inarudi Serikali kuu. Tukumbuke kuwa kuna sheria inazitaka mamlaka na wakala wa Serikali kutoa asilimia 10 ya pato ghafi kwenda Hazina na hivyo kinachobakia wakipiga mahesabu inaweza kushindwa kurejesha mkopo.
  12. HITIMISHO
  13. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa, kuwa maudhui ya muswada ni mazuri lakini jambo ambalo miaka yote tumekuwa tukiishauri Serikali kwamba, uvuvi wa bahari kuu ni sawa na mgodi ambao hauhitaji kuchimba au kuwekeza vifaa vikubwa na vyenye gharama kubwa zaidi ya meli husika,
  14. Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa uwekezaji ambao tumekuwa tukishauri ni kuwa na bandari ya uvuvi sambamba na kuwa na vifaa vya kuweza kutambua meli zinazovua kwenye eneo letu la bahari kuu bila ya kupewa idhini ya kufanya hivyo.
  15. Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa muswada huu umetambua umuhimu wa kuwa na vifaa ya kutambua shughuli za meli za uvuvi katika bahari kuu, jambo ambalo ni jema sana katika kuhakikisha rasilimali yetu hiyo inatumika kwa manufaa ya watanzania wote na sio vinginevyo.
  16. Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa baadhi ya vifungu vimewekwa ili kukinga wale ambao tayari walikuwa wanatakiwa nao kuwajibika kutokana na makosa yao, na hivyo kuwasafisha kupitia muswada huu,
  17. Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa sheria nzuri ni ile inayotungwa bila ya kuangalia mtu au kundi Fulani bali ni kwa mustakabali mpana wa jamii ya leo nay a kesho,
  18. Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa muswada wa sheria hii hautabadilisha mikataba na taratibu zote ambazo ziliingiwa kwa kutumia sheria inayofutwa,
  19. Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa kuendelea kutumia sheria na taratibu za mikataba ya sheria inayofutwa maana yake ni kuendelea na tatizo lile lile na inaweza kuchukua zaidi ya miaka mitano ijayo kabla matunda ya sheria mpya kupatikana.
  20. Mheshimiwa Spika, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia kwa makini maeneo ambayo yanaweza kuleta ugumu katika kukidhi madhumuni mapana ya utekelezaji wa sheria hii.
  21. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

……………..

Dr. Sware I. Semesi(Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

20.05.2020

Share Button