MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA WILLIE QAMBALO (MB), WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2018/19 NA MPANGO WA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO KWA MWAKA WA FEDHA WA 2019/2020

(Yanatolewa chini ya Kanuni za Bunge, Kanuni ya 99(9), toleo la mwaka 2016)

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika,napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi kwa kunipa afya na nguvu katika kipindi hiki kigumu sana katika ufanyaji wa siasa hasa kwa upande shindani na Chama Tawala na kuweka kusimama mbele ya hadhira hii ili kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
  3. Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani zangu za dhati kwa watanzania wote kwa kuionesha dunia kuwa haki hapa kwetu inanunuliwa!!! Kwa kitendo chao cha kuchanga kiasi cha shilingi 312 kwa muda wa siku tatu na kuhakikisha viongozi wote waandamizi wa CHADEMA wanakuwa huru. Asanteni sana watanzania wapenda haki!!!
  4. Mheshimiwa Spika,pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mwenyekiti wa Chadema Taifa na pia Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Hai, kwa imani yake kubwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nikisaidiwa na Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Mlimba. Kwa pamoja tunasema asante kwa imani hiyo kwetu.
  5. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu niwashukuru wananchi wote wa jimbo langu la Karatu kwa heshima na ushirikiano mkubwa walionipatia katika kipindi chote cha miaka mitano, ambacho nimekuwa Mbunge wao. Pia ni wapongeze wanachama wa CHADEMA kwa kusimama imara kwao na Chadema katika wimbi au upepo mchafu uliopita wa biashara ya kununua viongozi wa chama na Madiwani.
  6. Mheshimiwa Spika, Wizara hii kwa upana wake imeathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na janga la ugonjwa wa Corona lililoikumba dunia pamoja na mvua kubwa inayoendelea kunyesha ambapa barabara na madaraja vimearibika sana na hivyo kutokupitika katika maeneno mengi ya nchi. Madhara makubwa yamejitokeza sana kwenye sekta ya uchukuzi, pamoja na sekta ya ujenzi(barabara na madaraja) sekta ambayo huchangia mapato ya nchi kwa kiasi kikubwa sana. Hivi sasa usafiri wa anga kutoka nje ya nchi umesimama kabisa na hata usafirishaji kwa njia ya barabara nao umeathirika sana.
  7. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kutoa pole kwa wale wote ambao wameathirika na mlipuko wa ugonjwa huu wa Corona na wale wote walioathirika kwa mafuriko katika maeneno mbalimbali ya nchi.
  8. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nianze kupitia katika sekta zinazosimamiwa na wizara:
  9. MAJUKUMU YA SEKTA YA UJENZI
  10. Mheshimiwa Spika, Dira ya Sekta ya Ujenzi ni kuwa na barabara, madaraja, vivuko, viwanja vya ndege, nyumba na majengo ya Serikali na huduma za ujenzi zenye ubora wa kiwango cha juu, zenye gharama nafuu, zinazozingatia usalama na utunzaji wa mazingira.
  11. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Ujenzi kwa mujibu wa hati idhini ya Serikali imekabidhiwa majukumu ya kusimamia masuala yafuatayo ili kukidhi dira nzima ya ujenzi hapa nchini:
    1. Usimamizi wa Sera ya Taifa ya Ujenzi (2003) na utekelezaji wake pamoja na Sera ya Taifa ya Usalama Barabarani (2009) na utekelezaji wake;
    2. Ujenzi, Ukarabati na Matengenezo ya Barabara, Madaraja na Vivuko;
  • Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba na Majengo ya Serikali;
  1. Ujenzi na Ukarabati wa Viwanja vya Ndege;
  2. Usimamizi wa Masuala ya Ufundi na Umeme;
  3. Usimamizi wa Shughuli za Ukandarasi, Uhandisi, Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi;
  • Usimamizi wa Maabara na Vifaa vya Ujenzi;
  • Usimamizi wa Masuala ya Usalama na Mazingira katika Sekta ya Ujenzi;
  1. Uboreshaji Utendaji na Uendelezaji wa Watumishi wa Wizara; na
  2. Usimamizi wa Majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara.
  1. Mheshimiwa Spika, jukumu mojawapo la Wizara hii ni kusimamia sera tuliyojiwekea ya kuhakikisha miji yote mikuu ya mikoa nchini inaunganishwa kwa barabara za lami. Endapo serikali hii ingekuwa sikivu basi leo hii kazi hii ingeshakamilika. Uchambuzi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni umebaini kuwa kwa kipindi chote hiki serikali hii ya CCM imeshindwa kabisa kutekeleza sera hii kwani iko mikoa mingi ambayo bado haijaungwa kwa barabara za lami na pale ambapo kazi kidogo imefanyika tunaona inafanyika kisiasa zaidi. Mikoa ambayo haijaunganishwa hadi sasa ni Morogoro-Lindi, Morogoro-Njombe kupitia Mlimba, Arusha-Mara, Arusha-Simiyu, Mbeya-Singida, Rukwa- Katavi, Tabora- Kigoma, Katavi-Tabora, Mbeya-Njombe. Barabara hizi ambazo ni muhimu sana wakati mwingine hazipitiki kabisa na zinaleta usumbufu mkubwa kwa wasafiri na wasafirishaji. Mfano hai ni barabara inayounganisha mkoa wa Katavi na Tabora ina zaidi ya miezi miwili haipitiki kabisa
  2. Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mto wa mbu- Loliondo- Mugumu ambayo inaunganisha mkoa wa Arusha na mara iliingia kwenye kwenye ujenzi katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa kipande cha Loliondo – Sale (50Km) na hadi wa leo ni 40% tu ndiyo imekamilika. Yaani miaka minne serikali imejenga kilomita 20 tu na hivyo kwa spidi hiyo tunahitaji miaka  mingine  10 ili  kukamilisha barabara hiyo.
  3. Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika Randama utaona serekali ikisema inatafuta fedha kujenga barabara Fulani. Serikali hii imekuwa ikijinasibu kuwa ina fedha za kutosha sasa kama fedha zipo kwa nini msikamilishe barabara zetu? Ni dhariri sasa serikali hii imeshindwa kutekeleza mmoja ya miradi muhimu sana ya kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami na hivyo basi Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali ya CCM ipishe ili wengine wenye kuweza waje.
  4. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa pili wa miaka mitano uk.53 na 54 unaonesha kuwa sekta ya ujenzi hadi mwaka 2020 imewekewa lengo la kukua kwa kiwango cha asilimia 9.6, mchango wa sekta  kwenye pato la taifa uwe ni 11.8% na sekta iweze kuchangia asilimia 3.7 ya ajira zote. Aidha makampuni ya ndani katika kupata kazi za ujenzi iwe ni asilimia 60 ya thamani ya jumla ya kazi ujenzi hapa nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua katika malengo hayo tuliyojiwekea hadi sasa tumeyatekeleza kwa kiwango gani?
  5. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2019/20 Serikali imepanga kutumia Shilingi trilioni 1.4 katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 1.1 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 304.1 ni fedha za nje. Hadi Februari, 2020 jumla ya fedha zilizopokelewa ni Shilingi bilioni 862.412 sawa na asilimia 62.26 ya kiasi kilichoidhinishwa. Kati ya hizo, Shilingi bilioni 586.42 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 275.991 ni fedha za nje. Aidha, kati ya fedha za ndani ziizotolewa, Shilingi bilioni 403.165 ni fedha za Mfuko wa Barabara na Shilingi bilioni 183.25 ni kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.
  6. Mheshimiwa Spika, kati ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta ya ujenzi ya shilingi  trilioni 385,  kati ya fedha hizi kiasi cha shilingi  trilioni 1.223  ziliidhinishwa kwa ajili ya miradi ya barabara na madaraja tu. Ambazo ni sawa na 88.28% ya fedha zote za miradi kwa sekta ya ujenzi. Na hadi kufikia mwezi februari 2020 hazina ilikuwa imetoa jumla ya shilingi 671,410,826,457.17 (Bilioni 671.4)  sawa na 54.9%
  7. Mheshimiwa Spika, mvua zilizonyesha na zinazoendelea kunyesha nchini kote zimeharibu sana miundo mbinu ya barabara na madaraja kiasi kuwa barabara nyingi hivi sasa zinapitika kwa shida sana. Tunaona kuna udhaifu mkubwa serikalini wa kupeleka fedha za matengenezo kwa wakati na kwa viwango kidogo. Ni muhimu sana Watendaji wa TANROADS ngazi ya mikoa wanapewa mafungu ya kutosha ya kurudisha mawasiliano pale ambapo athari za mvua zinakuwa kubwa. Ni suala la uonevu mkubwa na ni dhambi kumwajibisha mtendaji wa wakala wa Mkoa kwa barabara iliyoharibika au daraja inayokatika wakati serikali haijapeleka fedha. Mnatarajia ajenge kwa fedha zipi?.
  8. Mheshimiwa Spika,ukiangalia miradi takriban asilimia 80 ya barabara sio miradi mipya, ni kiradi ambayo ilianza kujengwa wakati Mheshimiwa Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, kwa maana nyingine wakati wa awamu ya nne. Hadi sasa miradi hiyo inaendelea kwa kusuasua. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema ni vyema tukajikita katika azma ya kutenga pesa kumalizia au kutekeleza miradi hiyo kwa awamu awamu badala ya kugawanya kidogo kidogo ili kila mradi upatiwe mgawo.
  9. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa ujenzi wa barabara unaweza kukamilika vyema sana, ikiwa Serikali itaacha kufanya siasa ya kuridhisha kila mwanasiasa, jambo ambalo linaondoa maana halisi ya ujenzi wa barabara na kuwa ni jambo la kisiasa zaidi. Hivyo basi, jambo hilo kuendelea kulitia taifa hasara zaidi kwani miradi haimaliziki kwa wakati uliopangwa.
  10. Mheshimiwa Spika, kuna hiki kitu kinaitwa Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika takwimu za utekelezaji wa bajeti ya 2019/20 kimechukua fedha nyingi sana, kwa mfano; barabara za Pugu-Kifuru-Mbezi Mwisho-Mpigi Magoe-Bunju zimetumia shilingi milioni 20; Kigoma Lusahunga shilingi bilioni 1.365; Singida –Babati- Minjingu milioni 240.00; Dar-Mbagala-Gerezani, bilioni 3.5; Babati bypass ya KM 12, Bilioni 1.1; Nachingwea-Liwale KM 130, Bilioni 23.32
  11. Aidha, Mheshimiwa Spika, miradi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inayotekelezwa kwa kutumia fedha za mfuko wa barabara ni jumla ya shilingi bilioni 14.919. Pia mifumo ya Komputa kwa ajili ya usanifu wa barabara na kuandaa mipango ya usafiri jumla ya shilingi milioni 139.483
  12. Mheshimiwa Spika, hii ni kutaka kuonesha kuwa kuna fedha nyingi sana zinatolewa kwenye hii sehemu ya Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa fedha hizo kuna uwezekano mkubwa zikawa ni “kichaka cha kupitishia fedha za walipa kodi”. Kwa mazingira ya kawaida ni nani anafanya ukaguzi katika eneo hili? Na pale kazi hiyo inapomalizika inachukua muda mrefu miradi yenyewe kuanza kutekelezwa, na tukumbuke kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya kiuchumi kwa nchi yetu huo upembuzi yakinifu unaweza kupitwa na wakati kutokana na mambo tajwa hapo awali.
  13. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa kama Serikali haina fedha za kutekeleza miradi husika, ni kupoteza fedha kufanya kazi ambayo haionekani kama imefanyika au la, hivyo basi, kazi hiyo ifanyike na kukamilika na fedha za kuanza ujenzi ziwepo tayari na tuondoe siasa katika miradi ya ujenzi kwa kutaka kumridhisha kila mtu bila ya kuangalia hali halisi ya fedha iliyopo.
  14. Mheshimiwa Spika, Ukurasa wa 63 wa Ilani ya CCM aya ya “g” inasema kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara maeneo ya Chang’ombe, uhasibu, Morocco, Mwenge, Magomeni, tabata. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza ujenzi huo ulioanza kwa mujibu wa Ilani yenu umefikia wapi?

Wakala wa Ujenzi wa Barabara(TANROADS)

  1. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa za TANROADS za June 2019,mtandao wa barabara zilizoko chini ya ni kilomita 36,258 ambapo barabara kuu ni kilomita 12,178na barabara za mikoa ni kilomita 24,082. Katika mtandao huo wa barabara kuu, ziliozojengwa kwa lami ni 8,264km  wakati katika barabara za mikoa zenye lami ni 1,687 na bila lami ni 22,395km sawa na 93%
  2. Mheshimiwa Spika, TANROADS hufanya tathmini ya barabara zake kila robo mwaka jambo ambalo tunaunga mkono lakini tathmini bila mpango kabambe wa kuhakikisha barabara ninadumu ni kazi bure. Kambi rasmi bungeni inaitaka Serikali kuiwezesha TANROADS kuhakikisha barabara zote chini yao zinapitika muda wote. Haina maana kabisa TANROADS pupewa 70% za fedha za mfuko wa barabara wakati barabara zao zingine ni mbovu kuzidi za TARURA wanaopewa 30%,

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) 

  1. Mheshimiwa Spika,Jukumu kuu la Wakala wa Majengo ni usimamizi na uendeshaji wa miliki ya Serikali ikiwa ni pamoja na kupata viwanja kwa matumizi ya Serikali, kujenga nyumba za Serikali, kutunza nyumba na majengo ya Serikali, kutekeleza utaratibu wa kujenga na kuwauzia Watumishi wa Serikali nyumba za kuishi, kuwapangishia Watumishi wa umma nyumba za Serikali na kupangisha baadhi ya nyumba hizo kibiashara. Aidha, Wakala inasimamia miradi ya ujenzi na kutoa huduma ya ushauri kwa majengo ya Serikali.
  2. Mheshimiwa Spika, Katika Maboresho ya Utumishi wa Umma (public Service Reforms) majukumu ya TBA yalibadilishwa kutoka ujenzi na kuwa Manager na Msimamizi wa miradi ya ujenzi ya Serkali kwa sababu uwezo wao ulikuwa duni na kukosa ubora. Awamu ya tano, bila kujali sababu zilizofanya TBA kubadilishiwa majukumu na kuwa Maneja na msimamizi wa miradi ya ujenzi kwa niaba ya serkali, wamerudishiwa tena jukumu la kujenga na kujisimamia. Miradi mingi ya ujenzi ya TBA imekuwa ni duni na kukosa viwango na pia inachukua muda mrefu kukamilika. Kambi Rasmi ya Upinzani, inapendekeza kwamba, kutokana na uwezo mdogo wa TBA, na kutokana na ukweli kwamba hawawezi kujenga na kujisimamia, Serkali itafakari upya majukumu ya TBA na kuzingatia mabadiliko yaliyofanyika wakati wa Reforms. TBA ibakie kuwa Maneja na Msimamizi wa miradi ya ujenzi ya Serkali.
  3. Mheshimiwa Spika, ukiangalia wakala huyu anapewa miradi mingi na mikubwa, lakini ukweli ni kwamba kitendo cha kupewa miradi bila ya ushindani wowote maana yake ni kuua ushindani na kuwafanya wao wasiwe wabunifu zaidi.
  4. Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kuwa TBA wanarundikiwa kazi nyingi bila ya kuomba na kwa kuwa uwezo wao ni mdogo, jambo hilo linasababisha ucheleweshaji wa Utekelezaji wa Miradi mingi wanayopewa kuitekeleza au inatekelezwa chini ya kiwango. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ya mwaka 2018 iliyotolewa februari 2019, kuhusu utendaji wa TBA inaeleza yafuatayo;

 

  1. Mheshimiwa Spika,Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ilipewa majukumu ya ujenzi wa majengo na Taasisi mbalimbali za Serikali kwa mikataba yenye gharama za takribani shilingi 24,068,482,278. Uchambuzi wa Kamati ulibaini na kuthibitisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa Miradi husika.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Katika kushughulikia hoja ya TBA kutokamilisha Miradi kwa wakati, Kamati ilibaini dosari zifuatazo ambazo ndio sababu za kutokuwepo na ufanisi wa kutosha katika Wakala husika:

 

  1. Katika baadhi ya Miradi, vifaa vya ujenzi vilivyotolewa havikuwa vimepimwa na Wahandisi wa Miradi kwa kuzingatia makisio ya gharama za ujenzi (BOQ)17. Tafsiri ya jambo hili ni kwamba, thamani ya gharama zilizokuwa zinatolewa katika Miradi mingi ya TBA hazikuwa zinaakisi kazi iliyokuwa imefanyika hivyo kuleta ugumu wa kufanyika malipo kwa wakati.

 

  1. Kuhamishwa kwa vifaa vya ujenzi kutoka Mradi mmoja kwenda Mradi mwingine. Jambo hili limesababisha ucheleweshaji wa kukamilika Miradi mingi kwa muda uliopangwa.

 

  • Upungufu mkubwa wa wataalamu na vifaa. Kwa mfano, Kamati ilibaini kuwa Miradi miwili ilikuwa inasimamiwa na Mratibu mmoja kwa wakati mmoja.Aidha, katika Miradi mingi vifaa vya ujenzi vilikuwa vinachangiwa kwa wakati mmoja.

 

  1. Mheshimiwa Spika,Taarifa ya CAG ilibainisha baadhi ya Miradi ambayo TBA imeshindwa kukamilisha kwa wakati. Mfano ni Mradi wa ujenzi wa nyumba za “Magomeni quarters” wenye thamani ya shilingi bilioni 20 na Mradi wa ujenzi wa nyumba za Askari Magereza -Ukonga Dar es Salaam wenye thamani ya shilingi bilioni 10.Katika Mradi wa nyumba za Askari Magereza Ukonga, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua Mradi huo utekelezwe na Jeshi baada ya TBA kushindwa kuutekeleza ipasavyo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Miradi hiyo miwili ilianza kutekelezwa tarehe 01 Oktoba, 2016 na mwezi Machi, 2017 mtawalia. Aidha, Miradi yote miwili ilitakiwa kukamilika tarehe 15 Februari, 2018 na tarehe 05 Juni, 2018 mtawalia.Mheshimiwa Spika, Mwezi Januari, 2019 uhakiki wa CAG katika Miradi husika ulibaini dosari kadhaa. Mathalani, katika Miradi yote ilibainika hali ya utekelezaji wa Miradi ilikuwa katika hatua ya kuweka zege katika ghorofa ya kwanza na ya nne. Hali hii ilikwenda kinyume na Mkataba kwani kwa kipindi hicho muda wa utekelezaji wa Miradi husika ulikuwa umekwishakamilika.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Miradi mingine inayotekelezwa na TBA na ambayo ina dosari za utekelezaji ni pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Songwe, Makao Makuu ya TANROADS -Dodoma, Jengo la Tume ya Maadili -Dodoma, Jengo la Tume ya Uchaguzi –Dodoma, Jengo la Halmashauri ya Mji –Tarime, Jengo la Halmashauri ya Wilaya –Butiama na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa –Geita[1]

 

  1. Mheshimiwa Spika, kambi Rasmi ya Upinzani inauliza, inakuwaje, licha ya kasoro zote za utendaji kazi wa TBA bado Serikali inaendelea kuipatika kazi bila kufuata njia za kisheria za ushindani?
  2. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kama TBA inapatiwa kazi nyingi za Serikali, sekta binafsi itakua namna gani wakati haipewi kazi za Serikali?
  3. Mhshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina mashaka makubwa kuhusu utaratibu huu wa kurundika miradi kwa TBA na kuwalipa kabla ya kazi kumalizika au kwa kazi ambayo ina ubora wa chini, kwamba inaweza kuwa ni njia moja wapo ya kufanya ufisadi mkubwa wa fedha za walipa kodi.
  4. Mheshimiwa Spika, fungu 98 lina idara au taasisi nyingi, lakini umuhimu mkubwa ni utolewaji wa fedha za maendeleo, inavyoonekana kuwa ujenzi kwa miradi mingi kama vile viwanja vya ndege inatekelezwa zaidi kisiasa zaidi ya kuangalia uhalisi wa uchumi katika maeneo husika. Mifano ni mingi wa viwanja vya ndege ambavyo vimetumia fedha nyingi lakini sasa hivi yamekuwa machungio ya mifugo.Kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani imejikita katika maeneo ambayo tunadhani yana matatizo makubwa katika matumizi ya fedha za walipa kodi.
  5. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/21 KWA AJILI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
  6. Mheshimiwa Spika, kuhusu Bajeti ya Miradi ya Maendeleo, ujenzi fungu 98 kwa mwaka wa fedha 2020/21, imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 1.77 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 1.252 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 514.081 ni fedha za nje. Aidha, kati ya fedha za ndani Shilingi bilioni 641.746 ni fedha zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya Mfuko wa Barabara. Hivyo, fedha za kutekeleza miradi ya Barabara, Viwanja vya Ndege, Vivuko, Nyumba na Majengo ya Serikali, Usalama na Mazingira ni Shilingi bilioni 610.476
  7. Mheshimiwa Spika, fedha zinazoombwa kwa mwaka 2020/21 ni nyingi kwa shilingi bilioni 381.033 kwa kulinganisha na shilingi trilioni 1.385 zilizokuwa zimeidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2019/20.
  8. Mheshimiwa Spika, ni vizuri kutenga fedha, lakini ni vizuri mno kutenga fedha kulingana na uhalisia wa mapato yetu. Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fungu 98, utekelezaji wake haukuwa wa asilimia mia, sasa kutokana na sababu hiyo ya kutokuwepo kwa upatikanaji wa uhakika wa fedha na pia kutokana na mdororo wa ukusanyaji wa mapato yetu ni dhahiri kwamba Bajeti hii ina nia ya kuongeza madeni kwa Serikali kutoka kwa wakandarasi.
  9. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaiasa Serikali kupanga kulingana na kile kilichokuwepo au chenye uhakika wa kupatikana, kinyume cha hapo ni kushindwa kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake.
  10. Mheshimiwa Spika, aidha kwa ongezeko hilo na kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, kuna uwezekano mkubwa kuwa fedha hizo zikawa ni muendelezo wa kuficha fedha za kwa ajili ya kukisaidia chama tawala.
  11. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani mara zote ni mhamasishaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na pia ubia na serikali wa Build, Operate and Transfer-(BOT) kama ambavyo ilifanyika katika ujenzi wa daraja la Kigamboni. Tunaamini kwa mfumo huu wa uhusishwaji wa sekta binafsi au ubia katika ujenzi wa miradi mikubwa utasaidia kupunguza gharama zisiso na ulazima kwa Serikali. Kambi rasmi ya upinzani inajiuliza ni kwa nini miradi ya aina hii haifanyiki katika nchi hii ili hali kwa nchi za wenzetu tunaona ni miradi iliyofankiwa sana. KADCO imewasilisha serikalini miradi mitatu ya BOT mwaka jana lakini serikali iko kimya. Hizi ni fursa ambazo hatutakiwi kupoteza.
  12. SEKTA YA MAWASILIANO –FUNGU 68
  13. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 144 la tarehe 22 Aprili, 2016. Sekta ya Mawasiliano inahusika kuandaa, kusimamia na kuratibu masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha kuwa TEHAMA inachangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi yetu.
  14. Mheshimiwa Spika, sekta hii ya mawasiliano inasimamia taasisi sita zenye majukumu tofauti lakini yanashabihiana, ambazo ni;
  15. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tanzania Communication Regulatory Authority – TCRA)
  16. Shirika la Mawasiliano Tanzania (Tanzania Telecommunicatios Corporation – TTCL)
  • Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC)
  1. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (Universal Communications Service Access Fund – UCSAF
  2. Shirika la Posta Tanzania (Tanzania Posta Corporation – TPC)
  3. Tume ya TEHAMA (ICT Commission – ICTC)
  4. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa taasisi hizo tajwa pamoja na wizara zinatekeleza wake majukumu yake ipasavyo na hivyo kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu taasisi hizi Katika Mwaka wa Fedha 2019/20 zilipanga kukusanya jumla ya Shilingi bilini 470.136. Hadi kufikia tarehe 29 Februari, 2020. Taasisi zote zilikuwa zimekusanya jumla ya Shilingi bilioni 258.87 Sawa na asilimia 55 ya lengo.
  5. Mheshimiwa Spika, kati ya hayo makusanyo, Mamlaka ya udhibiti wa mawasiliano TCRA ilitakiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 141.369  ambazo ni sawa na 30.06%.; TTCL ilitakiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 196.832 sawa na 41.86%
  6. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wadau wa kutoa huduma au service providers wanakuwa tayari wameumizwa, kinachofuata mlaji wa mwisho anaibiwa yeye bila kufahamu, mfano mzuri ni pale tunaponunua kifurushi (bundle) cha siku, wiki au mwezi utasitishiwa matumizi bila ya mhusika kutumia vifurushi hivyo, hii pia inatokana na kutokusimamia Mfumo wa kuhakiki wa huduma ambayo sisi wateja tunapatiwa kama ni stahiki kutokana na huduma za mawasiliano na fedha tunazolipa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Mamlaka kuangalia upya jinsi mfumo wa vifurishi iwe vya maongezi au data, kwani kuna hujuma kubwa dhidi ya wateja.
  7. Mheshimiwa Spika, mamlaka ya udhibiti wa mawasiliano (TCRA) ndiye ambaye kulingana na majukumu yake anayezalisha fedha nyingi katika utendaji kazi wake, lakini katika kufanya hivyo kumekuwepo na maumivu makubwa sana kutoka kwa wateja wake. Faini ambazo zinatolewa bila kuangalia hali halisi kwa mhusika ili mradi tu fedha zinatakiwa ni kupeleka maumivu kwa wahusika ambayo maumivu hayo yanarudishwa kwa wateja bila ya wao kufahamu.
  8. Mheshimiwa Spika, kati hilo ndio maana kati ya fedha zilizowekewa lengo kukusanywa kiasi cha shilingi bilioni 141.369 kwa mwaka wa fedha 2019/20, hadi mwezi februari 2020 zilikuwasanywa shilingi bilioni 129.993 sawa na 91.95%
  9. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano, imeendelea na zoezi la usajili wa laini za simu kwa njia ya biometria ambapo hadi tarehe 10 Machi, 2020 idadi ya laini zilizosajiliwa zilikuwa 35,813,455 sawa na asilimia 83.1 ya laini zote 43,072,868 zilizounganishwa mitandaoni.
  10. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kuwa laini zilizozimwa hadi kufikia tarehe 10 Machi, 2020 zilikuwa 5,886,286. Aidha, laini ambazo bado hazijasajiliwa kwa alama za vidole lakini zilisajiliwa kwa kitambulisho cha Mpiga Kura na kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi ni laini 7,259,413.  Uhakiki unaendelea kwa kushirikiana na NIDA kwa ajili ya taratibu za kuzifungia.
  11. Mheshimiwa Spika, wakati huo huo tunaambiwa kwa mwaka miamala 2,004,196,139 yenye wastani wa fedha zilizopita ni shilingi trilioni 12.203. Hii ikiwa na maana kwamba laini hizo milioni 43 ndizo zilipitisha kiasi hicho cha trilioni 12.203. tukichukulia kuwa kiasi hicho kinakatwa kodi ya ongezeko la thamani la 18%. Hii ni dhahiri kuwa Serikali ilipata fedha nyingi kutokana na chanzo hiki. Kiasi hicho ni miamala tu, bado muda wa maongezi ambao pia unakatwa kodi.
  12. Mheshimiwa Spika, kwa mahesbabu hayo hayo, tukichulia lini ambazo zimefungiwa 5,886,286 zingepitisha miamala kiasi gani na kiasi gani cha kodi kingekatwa katika muda wa maongezi? Hivi ni kwanini Serikali inakuwa ndio mchawi mkubwa wa uchumi wetu?
  13. Mheshimiwa Spika, tukumbuke kuwa katika usajili wa laini za simu mahitaji hayakuwa ni kitambulisho cha URAIA tu, bali ilikuwa ni vitambulisho vya, leseni ya udereva, kitambulisho cha mpiga kura na hati ya kusafiria. Tukumbuke kwamba vitambulisho vyote hivyo vinapatikana kwa njia ya utambulisho wa vidole. Sasa ulazima wa kitambulisho cha uraia ni mbinu ambayo hadi sasa tunashindwa kuelewa ili lenga nini hasa!
  14. Mheshimiwa Spika, Kama ilivyoanishwa kwenye sheria ya EPOCA ya mwaka 2010 na Kanuni za Sheria hiyo za mwaka 2011, masharti ya usajili wa laini za simu ni kama ifuatavyo: 1.Mtoa huduma au wakala analazimika kujaza fomu ya usajili; 2.Mteja Mtarajiwa anatakiwa kuonyesha mojawapo ya vitambulisho halisi vyenye picha yake; Pasipoti, Kitambulisho cha kazini, Leseni ya udereva , Kadi ya usajili wa Mpiga Kura, Barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mitaa ikiwa na picha, Kitambulisho cha Taifa, Kitambulisho cha SACCOs, au Kadi ya benki yenye picha. Kimojawapo kati ya hivyo vyote kitakuwa ni sahihi katika usajili wa laini ya simu.
  15. Mheshimiwa Spika, hasara ambayo wenye namba zao zimefungiwa wakiamua kuishtaki mamlaka kwa kuvunja sheria yake kuhusiana na usajili italazimika kulipa fedha nyingi mno, kwani sheria iko wazi.
  16. SHIRIKA LA MAWASILIANO TANZANIA (TTCL)
  17. Mheshimiwa Spika, randama ya mwaka 2020/21 inaonesha Katika mwaka wa fedha 2019/20 Shirika lilikadiria kuzalisha na kukusanya mapato ya Shilingi bilioni 196.832 kutokana na huduma za Shirika ambazo ni simu, data na kupangisha maeneo kwa ajili ya vyombo vya mwasiliano. Lakini hadi kufikia tarehe 29 Februari, 2020, Shirika limekusanya jumla ya Shilingi bilioni 60.137 sawa na asilimia 30.5 na matumizi ya Shirika ni Shilingi bilioni 66.718
  18. Mheshimiwa Spika, kwa mizania hiyo ya mapato na matumizi ya TTCL ni kwamba shirika limefanya kazi kwa hasara ya shilingi bilioni 6.581
  19. Mheshimiwa Spika, makusanyo hayo ya 30.5% ya makisio makuu ya makusanyo ya TTCL ndiyo yanayokwenda hadi kwenye bajeti kuu ya Taifa, jambo hili linasababisha hata bajeti yetu miaka yote utekelezaji wake uendelee kuwa na upungufu mkubwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa suluhu ya jambo hili ni kuhakikisha tunapanga kutokana na hali halisi. Shirika lingeweza kabisa kufanya vyema kama watendaji wasingetoa “gawio- dividends”  kwa Serikali wakati shirika linamahitaji makubwa ya uwekezaji. Hii ni kushindwa kwa utawala wa shirika na ni kwanini hadi sasa “menejiment” ya TTCL bado ipo ofisini?
  20. Mheshimiwa Spika, kuhusu utendaji kazi wa TTCL kuwa wa kibiashara na hivyo kushindana na makampuni mengine yanayotoa huduma kama zake, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kurekebisha sheria zilizoanzisha Kampuni hiyo ili ziendane na wakati na kufanyakazi katika mazingira ya ushindani kuliko ilivyo sasa. Utendaji wake ni wa kiukiritimba mno kiasi kwamba, menejimenti yake haiwezi kuamua sula lihusulo uwekezaji bila idhini ya bodi, tukumbuke kuwa biashara ni muda.
  21. SEKTA YA UCHUKUZI- FUNGU 62.
  22. Mheshimiwa Spika, sekta ya uchukuzi inahusika na usafirishaji wa njia ya anga, njia za majini (bahari na maziwa), njia ya reli na njia ya barabara. Pia, inahusika na mamlaka za udhibiti za uchukuzi na usafirishaji.
  23. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 sekta ya uchukuzi ilitengewa jumla ya shilingi trilioni 3 zikiwa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi mwezi Februari 2019 fedha zilizopokelewa na sekta husika ni shilingi bilioni 391.162 sawa na asilimia 17 tu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Aidha, Randama inaonesha kuwa kuna fedha zilizokuwa zimebakia kwenye  akaunti ya Amana kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyokuwepo na hivyo kufanya fedha za maendeleo kuwa shilingi bilioni  947.723
  24. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2019/20 kwa miradi ya Maendeleo iliidhinishiwa jumla ya shilingi trilioni 3.544 kati ya fedha hizo shilingi trilioni 948 sawa na asilimia 81.22 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo katika sekta hii ilikuwa ni kwa ajili kuimarisha reli hapa nchini.
  25. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara fungu 62 inaomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi trilioni 3.068 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Kati ya Fedha hizo, Shilingi trilioni 2.938 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 129.989 ni fedha za nje. 
  26. Mheshimiwa Spika, miradi mikubwa ambayo inatarajiwa kuendelea utekelezaji wake ni pamoja na Ujenzi wa reli mpya ya Standard Gauge, Ufufuaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania na Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu. Aidha, maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2020/21 ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya Reli iliyopo, upanuzi wa Bandari, Huduma za Usafiri wa nchi Kavu na kwa njia ya Maji na Usafiri wa Anga.
  27. Mheshimiwa Spika, wizara ya uchukuzi ina maeneo matatu makubwa ambayo ni reli, ndege na bandari. Kwa muktadha wa mambo hayo yote Kambi Rasmi ya Upinzani inapata shida kutoa maoni yake katika eneo la shirika la ndege la Taifa-ATCL pamoja na bandari zetu za kwenye maziwa na meli zake.
  28. Shirika la Ndege la Taifa-ATCL
  29. Mheshimiwa Spika, Serikali imekua ikinunua Ndege kwa ajili ya kulifufua Shirika la Ndege la ATCL. Lakini kutokana na hali halisi kuwa hizo ndege zinazonunuliwa na jinsi zinavyofanya kazi na kuhudumiwa sio jukumu la ATCL bali ni la Ofisi ya Rais fungu 20.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kitendo cha mkaguzi na mdhibiti Mkuu kushindwa kufanya ukaguzi juu ya mchakato mzima wa manunuzi na utendaji kazi wa ndege hizo mpya ambazo zina nembo ya ATCL lakini haziko kwenye umiliki wa ATCL linatupa sisi Kambi Rasmi na pengine Bunge zima ugumu wa kuhoji.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa shirika la ndege kwa kweli halijafufuliwa kwani bado halina ndege hata moja bali ni wakala wa Ofisi ya Rais Ikulu fungu 20 katika kufanya biashara.
  2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuwa ili hoja ya kulifufua shirika la taifa la ndege la taifa iwe na mashiko, ni vyema ndege zote zilizonunuliwa zimilikiwe na shirika la ndege na shirika liwe na uwezo wa kuziendesha bila kuingiliwa na Serikali na liweze kujiendesha kibiashara na kuwajibika kwa Mkaguzi na mamlaka zingine kwa mujibu wa sheria. Vinginevyo hizi tambo za kufufua shirika hazitakuwa na maana.
  3. Kilimanjaro Airport Authority (KADCO)
  4. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa katiba ya kampuni (Memorundum and articles of association) KADCO ni kampuni ya umma iliyopewa jukumu la kuendesha na kuendeleza kiwanja cha KIA. Kampuni hii imetekeleza wajibu wake ipasavyo na mafanikio yanaonekana ikiwa ni pamoja na kampuni kujiendesha na pia kutoa gawio serikalini mwaka hadi mwaka mfano katika mwaka wa jana walitoa gawio la 1.0 Bilioni. Hata hivyo zipo changamoto ambazo zinakwamisha jitihada za kampuni hiyo kufanya vizuri zaidi.
  • Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
  1. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imezungukwa na nchi zingine sita ambazo hazina mlango wa bahari, bado tuna bandari zinazo hudumia katika maziwa makuu, ambayo pia yana ushirika na nchi zingine. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona hiyo ni fursa muhimu sana ambayo tungeitumia vizuri mapato yetu kupitia sekta hii yangekuwa makubwa sana. Kwa muktadha huo umuhimu wa kuimarisha bandari zetu na meli zetu uko wazi.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa suala la ujenzi wa bandari zetu na ununuzi au matengenezo ya meli zetu jambo hilo liko chini ya ujenzi fungu 98, kwa muktadha huo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona wizara fungu 62 haina hoja na suala lililo bakia kwa wizara yetu ni mizigo na abiria tu. Hivyo basi, kwa muktadha huo kilichobakia na utendaji wa Bandari ya DAR na bandari za Tanga, Mtwara jambo ambalo kwa sasa linatia wasiwasi mkubwa kulingana na mazingira ya biashara duniani yalivyo.
  3. Mheshimiwa Spika, kuhusu upanuzi wa bandari kwa ujenzi wa magati mapya Kambi Rasmi ya Upinzani tumeishaongelea sana na kutoa ushauri, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu kulingana na vipaumbele vya Serikali kuwa katika maeneo mengine ambayo sio hayo.
  4. Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo nalo limekuwa ni tatizo ambalo ufumbuzi wake umeachwa mikononi mwa Ikulu, japokuwa kwenye mpango wa maendeleo ya miaka mitano linaonekana kuwa utekelezaji wake unatakiwa ufanyika ndani ya kipindi hiki.
  5. Kampuni ya meli ya Serikali ya Tanzania na China (SINOTASHIP)
  6. Mheshimiwa Spika, SINOTASHIP yenye makao yake makuu Dar es Salaam ni kampuni ya pamoja  kati ya Serikali ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania na Serikali ya jamhuri ya watu wa China kwa uwiano wa 50;50. Kampuni hii iliyoanzishwa mwaka 1967, msingi wake mkuu ulikuwa ni kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi wanahisa.
  7. Mheshimiwa Spika, wakati wa kuanzisha kampuni hii serikali ya Tanzania ilikopeshwa na mwanahisa mwenza kiasi cha cha paundi milioni mmoja na nusu (Pound 1,500,000) kama mtaji wa kununua meli nne za mizigo mchanganyiko( General Cargo), na wachina wao walitoa kiasi kama hicho hicho. Kumbukumbu zilizopo ndani ya kampuni hazionyeshi kama Tanzania imerejesha mkopo huo au kama tumesamehewa deni hilo. Serikali iwaambie watanzania ukweli wa jambo hilo ili tujue kama tuna chetu kwenye kampuni hiyo. Kampuni hii inasuasua sana na pengine ni kwa sababu Tanzania tumezembea wajibu wetu ikiwa pamoja na kurejesha mkopo huo.
  8. Mheshimiwa Spika, Serikali pia ituambie faida tuanayoipata kama nchi kwa kuwa na kampuni hiyo ya ubia ilihali kampuni haijawahi kutoa gawio serikalini. Kampuni hiyo kwa sasa inamiliki meli mmoja tu “MV Changshun II” ambayo tena ilikopwa  na moja ya changamoto kubwa ya kampuni hiyo ni ukosefu wa fedha za kulipia deni la mkopo huo ambao kwa sasa ni dola za  kimarekani milioni 5.07.
  9. Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kuweka wazi utaratibu wa kulipa deni hilo ili Watanzania wajue kuwa wana sehemu yao katika kampuni hiyo.
  10. Shirika la reli-TRC
  11. Mheshimiwa Spika, katika usafiri wa Reli, kwa kipindi chote cha miaka minne, macho, masikio na fedha nyingi zinapelekwa katika ujenzi wa reli kwa kiwango cha kati (SGR). Ni wazo jema na lililo na umuhimu kwa watanzania walio wengi kwa maeneo mbalimbali ya nchi kulingana na matawi ya reli katika maeneo mengi.
  12. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilikwisha toa ushauri mara nyingi kwamba ujenzi wa SGR ungesubiri kwanza kuanza kazi kwa mradi wa uzalishaji wa chuma wa Liganga na Mchuchuma ili kupunguza gharama za kuagiza vyuma kwa ajili ya kutandika reli kutoka nje ya nchi. Jambo hilo la kuagiza vyuma linaifilisi nchi kwa kuondoa fedha za kigeni chache tulizo nazo. Lakini wazo hilo Serikali haikulifanyia kazi kwa sababu ambazo inazijua, lakini Kambi Rasmi ya Upinzani ina wasiwasi kwamba mradi huo wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kati (SGR) utashindwa kutekelezeka kwa muda uliopangwa, kutokana na hali halisi ya uchumi wa ndani na duniani ulivyo sasa.
  13. Mamlaka ya Reli-Tanzania na Zambia-TAZARA.
  14. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), mapato yake yameendelea kushuka mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2015/16 hadi sasa na hivyo kujiendesha kwa hasara. Hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na miundombinu chakavu hasa mabehewa ya mizigo na abiria, ukosefu wa mtaji, madeni makubwa. Tazara inadaiwa  zaidi ya shilingi bilioni 225.
  15. Mheshimiwa Spika, ni kwa miaka mingi sasa serikali imetoa ahadi ya kuiwezesha na kuibororesha Tazara na kubeba jukumu la kulipa mishahara ya watumishi wa Tazara kwa kile kinachoita kuwa Tazara haina uwezo wa  kujiendesha yenyewe, hii inafanya tazara kushindwa kuwalipa masaa ya ziada  na kulipa wayumishi wanaostaafu  na kupelekea maisha magumu kwa watumishi hao. kambi rasmi inataka majibu toka serikalini, lini shirka hilo lipewa uwezo wa kujiendesha lenyewe,  ni  lini Serikali itawalipa wafanyakazi masaa yao ya ziada, na serikali ina mkakati gani wa kulipa wastaafu  wote wa Tazara walistaafu  tangu mwaka 2005, 2009 hadi sasa.
  16. Mheshimiwa Spika, Serikali ione umuhimu wa kuiwezesha TAZARA haraka kwa uchumi wa nchi na kuokoa barabara za mikoa inayopita Tazara.
  17. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani hairidhishwi jinsi Serikali hizi mbili ambazo ni wabia wa TAZARA zinavyoichukulia TAZARA kama yatima. Reli hii ni fursa kubwa kwa usafiri na Usafirishaji kwa nchi karibu zote za SADC. Kama kweli nchi zetu zimeshindwa kuiendesha RELI hii ni kwanini tusiwatafute wabia wengine ambao wataona fursa hii na kuiendesha kwa faida?
  18. HITIMISHO
  19. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa; awamu hii ya Serikali imekuwa kinara katika kupeleka fedha kwenye ujenzi wa miundombinu, ambayo kukamilika kwake ni kutegemeana na hali ya uchumi wa dunia utakavyokuwa, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona;

Na kwa kuwa, miundombinu kwa kiwango kikubwa imekuwa ikichukua mabilioni ya shilingi za walipa kodi kwa gharama ya huduma nyingine za kijamii kama vile elimu, afya na maji; wakati huo ajira zinazotokana na uwekezaji huo ni ndogo;

Na kwa kuwa; makampuni yanayojihusisha na uwekezaji wa miundombinu hiyo ni kutoka nje na hivyo fedha zinahamishwa na nyingi aziingii kwenye mzunguko wetu wa uchumi, ujenzi wa SGR, Ujenzi Bwawa la kuzalishia umeme wa Maji kwenye Mto Rufiji na pamoja na ujenzi wa madaraja makubwa;

Na kwa kuwa uwekezaji mzuri na wa muda mrefu kwa nchi zote ziliezoendelea ulifanyika kwenye elimu au rasilimali watu na baadae ni kwa rasilimali vitu,

Na kwa kuwa; uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji unafanyika bila kuangalia rasilimali watu tuliyonayo katika sekta hiyo, ni dhahiri kwamba siku zijazo itatulazimu kama nchi kuanza kukodisha wataalam toka nje ili kuendesha miundombinu hiyo;

Na kwa kuwa; idadi kubwa ya watanzania imebakia kuwa muangaliaji na sio mshiriki katika uwekezaji huo, kwani manufaa ya uwekezaji ni kwa kikundi kidogo katika jamii yetu;

  1. Hivyo basi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema ni muda mwafaka sasa, Serikali ya awamu ya Tano ianze kujiandaa kisaikolojia kukabidhi madaraka kwa vyama shindani na Chama tawala, tunaamini kabisa uchaguzi hujao utakuwa rahisi sana kwani Serikali imevuruga sana na kuliaibisha taifa ndani na nje ya mipaka jambo linalotupatia urahisi zaidi wa kuiondoa madarakani. Duniani kote nguvu ya umma ndio silaha ya uhakika katika kufanya mabadiliko ya kweli na ya haki, msijidanganye na vyombo vya dola, kwani vyombo hivyo vinaendeshwa na kusimamiwa na umma huohuo ambao umedhalilishwa na kupuuzwa sana.
  2. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………….

WILLY QAMBALO (Mb)

MSEMAJI MKUU- KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO

.04.2020

[1] Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za  Serikali- Taari ya kazi za Kamati  2018,  iliyosomwa  februari, 2019

Share Button