TAARIFA KWA UMMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) kimeendelea kupokea kwa masikitiko makubwa misiba ya Wabunge na Watanzania wengine inayosababishwa na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

Kama ambavyo tumeshauri mara kadhaa, ni dhahiri hatua za ziada za dharura zinapaswa kuchukuliwa kupunguza kasi ya maambukizi na hivyo kuokoa, kadri iwezekanavyo, maisha ya Watanzania.

Wakati tukisubiri wenye mamlaka kuchukua hatua hizo, na kwa sababu Chadema tulishasisitiza kila mmoja wetu, kuwa mstari wa kwanza wa kujikinga na kukinga wenzake, Chama kinatoa maelekezo yafuatayo kwa wabunge wake wote:

1. Wabunge wote wa Chadema waache mara moja kuhudhuria vikao vya Bunge au Kamati za Bunge.

2. Wabunge wote wa Chadema kutokufika kabisa katika eneo lote la Bunge, Dodoma na Dar es Salaam.

3. Wabunge wote kujiweka katika karantini (self Isolation) kwa muda usiopungua wiki mbili.

4. Tunasisitiza Wabunge wetu walioko Dodoma wasiende majimboni/mikoani bali wabaki Dodoma kwenye karantini hadi itakapothibitika wao ni salama na au kupata maelekezo mengine yeyote yaliyo rasmi.

Aidha, tunawasihi Wabunge wengine wote wa vyama vingine kutafakari kama kweli ni salama kuendelea na Vikao vya Bunge katika mazingira yaliyopo.

Kwa msimamo huu, tunalitaka Bunge kuchukua hatua zifuatazo:

1. Kusitisha shughuli za Bunge kwa siku 21 kuruhusu Wabunge na Watumishi wote wa Bunge kwenda karantini.

2. Kupima Wabunge wote, Watumishi wa Bunge na familia zao kubaini ni wangapi tayari wana maambukizi ya virusi ili hatua stahiki za kitabibu ziweze kuchukuliwa.

3. Kamati mahsusi za Bunge hususan Kamati ya Huduma za Bunge na Kamati ya Uongozi zifanye vikao vyake kwa njia ya mtandao (zoom) ili maamuzi muhimu kuhusu Utawala na mwenendo wa Bunge yaweze kufanyika.

Chadema inaendelea kusisitiza kwa Watanzania wote kuwa: mstari wa kwanza wa kinga ( First line of protection) ni kila mmoja wetu.

Tunasisitiza, ni uzembe kusubiri kufanyiwa kinga na mwenzio. Anza kwako.

Freeman Aikaeli Mbowe (MP)
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na
Kiongozi wa Upinzani Bungeni
1 Mei, 2020

Share Button