1.0 Utangulizi:

COVID 19 (Corona Virus Disease of 2019) ni ugonjwa usio na tiba unaoitesa dunia kitabibu, kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Ni mlipuko wa ugonjwa unaosambaa kwa kasi na unaoua binadamu bila kujali mipaka ya nchi, rangi ya binadamu, tamaduni zetu, mifumo ya kisiasa na kijamii, jinsia na hata utajiri au cheo cha mtu na nafasi yeyote ya kimadaraka au mamlaka.

Ugonjwa huu ulianzia Jiji la Wuhan, nchini China Disemba 2019 na mwezi mmoja baadaye, mnamo 30 Januari 2020, ulitangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa “Public Health Emergency of International Concern”. Kuongezeka ghafla kwa maambukizi na vifo kulishika kasi kuanzia mwezi Machi, 2020. Tangu kutangazwa kwake kuwa janga la Dunia, ugonjwa huu umeshaambukiza watu zaidi ya milioni 3 na kusababisha vifo (vilivyotambulika rasmi) zaidi ya 203,000 duniani.

Tafiti za kisayansi na uzoefu wa nchi zilizotangulia kupambana na janga hili; na kwa mujibu wa taarifa rasmi za WHO, mtu mmoja anaweza kuambukiza watu 2.6 kwa siku na baada ya mizunguko 10 ya maambukizi yanayoweza kuchukua kati ya siku 5 – 6 ; wanaweza kuzalishwa wagonjwa zaidi ya 3500! Kasi hii inatisha.

Njia Kuu ya kisayansi ya kupunguza au kuzuia maambukizi haya ni “kuvunja mwingiliano wa watu (breaking the cycle of human interaction). Wengi wanautambua mfumo huu kama “lock down”. Ni njia ngumu na yenye gharama kubwa za kiuchumi hususan kwa nchi masikini na jamii zenye uwezo mdogo wa akiba na uchumi. Njia nyingine ni pamoja na kuvaa barakoa (masks), kunawa mikono, mara kwa mara, kwa sabuni na maji yanayotiririka, kutumia vitakasa mikono (sanitizer) mara nyingi iwezekanavyo, kuweka umbali baina ya mtu na mtu wakati wote (social distancing) nk.

Hakuna njia rahisi ya kukabiliana na janga hili. Ni chaguo kati ya haki ya mtu mmoja mmoja (individual right) dhidi ya usalama wa jamii (public safety).

Ni chaguo la kipi ni bora: kuvuruga uhuru wa kawaida wa watu wako kwa muda maalum na kupunguza maambukizi miongoni mwao (trade off peoples freedom for greater public good) au kuruhusu waendelee na taratibu zao za maisha za siku zote (business as usual) na kisha tuwe tayari kukabiliana na hatua isiyoepukika ya kufurika kwa wagonjwa, huduma za kitabibu kuzidiwa, kuambukiza wauguzi na madaktari na hatimaye kuzika watu wetu kwa mamia na maelfu.

Ni chaguo kati ya uamuzi wa kuulinda uchumi wa nchi yako au kulinda wananchi wako dhidi ya maambukizi na maangamizi ya maisha yao. Kimoja lazima kiwe kipaumbele.

Siku 100 za kwanza za ugonjwa huu zimejibu maswali mengi kupitia tafiti, uzoefu na hali halisi katika nchi mbalimbali. Kwamba hauna mipaka; tena hauchagui rangi ya binadamu; siyo ugonjwa wa matajiri; na tena hadi sasa hauna kinga au tiba na kwamba unaua kweli japo ukiumiza zaidi watu wenye umri mkubwa na wale wanaosumbuliwa na maradhi mengine makubwa kubwa.

Ni dhahiri basi, ugonjwa huu unahitaji juhudi za pamoja za kimataifa kuukabili. Ni ugonjwa ulioiweka dunia usawa mmoja. Namna kila nchi inavyoweza kuukabili ugonjwa huu kwa kiwango kikubwa sana unategemea namna nchi yenyewe ilivyoupokea na namna iliyoamua kuukabili katika mifumo yake ya kiutawala na kiutamaduni; namna ilivyopokea tahadhari za kisayansi za WHO na wataalam wa afya (initial response to the pandemic).

Pamoja na kuheshimu uhuru wa kuamini kwa watu na mataifa mbalimbali, vita dhidi ya Corona ni ya kisayansi na siyo ya kidini. Kutegemea Rehema za Mungu bila kuchukua tahadhari na mikakati ya kisayansi, kibajeti, kielimu na ushirikishwaji umma ni udhaifu mkubwa wa Watawala ambao utawalazimisha kubeba lawama huko tuendako.

Ni wajibu wa Watawala kutambua kuwa mapambano dhidi ya janga hili yanahitaji elimu na ushirikishwaji. Ni mzigo wa pamoja kati ya wafanya maamuzi (decision makers) na watekelezaji wa maamuzi (decision takers).

Ni ujinga uliopitiliza kwa nchi yeyote kufikiria ina uwezo wa kukabiliana na janga hili “kwa utaratibu wake wa ndani”. Iwe kwa misingi ya kiuchumi, kisayansi, kitabibu, kiutamaduni, kwa imani za kidini na mbaya zaidi hata kwa imani za kishirikina. Ni ujinga zaidi kutokujifunza kutoka kwa uzoefu wa nchi zilizotangulia kupambana na janga hili. Janga hili linahitaji dunia kupambana pamoja kwa kushauriana na kusaidiana. Watawala wasiotambua hili ni janga kubwa kwa watu wao sasa na siku za usoni, hakika wanajitayarishia na wanastahili anguko kubwa la kisiasa.

2.0 COVID19 na Tanzania

Mgonjwa wa kwanza wa Corona alitambulika nchini Tanzania, mkoani Arusha tarehe 16 Machi 2020. Hadi kufikia leo, ikiwa ni takriban siku 45 tangu kuripotiwa kwa mara ya kwanza, idadi ya walioambukizwa imeongezeka hadi kufika 480. Aidha, watu 16 wamepoteza maisha. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Serikali iliyotolewa mapema leo na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Tangu WHO ilipotangaza ugonjwa huu kuwa Janga la Dunia, Chama chetu kiliamini na kinaendelea kuamini katika ushirikishwaji wa Taifa zima katika kupambana na Janga hili. Tunaamini siyo sahihi hata kidogo kwa Serikali iliyopo madarakani “kuhodhi” vita hii kwa gharama ya maisha na uchumi wa Watanzania. Mataifa mengi yametumia utaratibu wa kuunda “National COVID 19 Task Force”.

Ushirikishwaji katika nchi za wenzetu chini ya uratibu wa Serikali umehusisha Wanasiasa, Mabunge ya nchi zao, taasisi mbalimbali za dini, taasisi za kitaaluma, wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta mbalimbali, vyama vya wafanyakazi, taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali za kitaifa na kimataifa, Wataalam wa Afya katika ujumla wao, Vyombo vya Habari, Jumuiya za Kikanda pamoja na wanazuoni kwa upande mmoja na wananchi kwa upande wa pili. Ushirikishwaji huu unafanywa kwa uwazi na taarifa mbali mbali kutolewa kwa wananchi bila kificho, ghiliba au udanganyifu.

Mimi binafsi, ni mhanga wa janga hili kwani mwanangu alikuwa miongoni mwa wahanga 10 wa kwanza. Aliambukizwa na kupelekea familia nzima kuwa chini ya karantini huku kijana akiendelea na uangalizi na matibabu hadi leo ikiwa ni takribani zaidi ya wiki 5.

Sisi kama chama, na tukiamini nguvu ya pamoja tuliamua kusitisha shughuli zetu za siasa zinazohusisha mikusanyiko mikubwa, kufuatia maelekezo ya serikali.

Kwa nyakati mbalimbali, binafsi nimezungumza suala hili na namna bora ya kushughulika kwa pamoja kupambana nalo. Nimezungumza na Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Spika wa Bunge na Naibu wake, mawaziri kadhaa moja kwa moja au kupitia kamati mbalimbali za kibunge, ikiwemo Kamati ya Bajeti, Kamati ya Uongozi wa Bunge na hata Tume ya Huduma za Bunge.

Aidha, viongozi wote waandamizi wa Chama chetu akiwemo Makamu wa Mwenyekiti Bara na Visiwani, Katibu Mkuu na Manaibu wake, Sekretariati ya Chama Taifa, Kamati Kuu ya Chama Chetu, Waziri Kivuli wa Afya na Naibu wake, wabunge kadhaa wa Chama chetu, bila kuwasahau viongozi wetu wa Mabaraza ya Chama ya BAZECHA, BAWACHA, BAVICHA, Viongozi wa Kanda za Chama, Mikoa, Wilaya, Majimbo na hata wanachama wa kawaida, wametoa ushirikiano na ushauri mwingi kwa Serikali kwa nia njema ya kuona Taifa likijumuika pamoja kupambana na janga hili.

Tunatambua vile vile juhudi zinazofanywa na vyama vingine vya siasa vya upinzani, hususan Chama cha ACT Wazalendo na Chama cha CUF, taasisi mbalimbali za dini, taasisi mbalimbali za kiraia na kitaaluma, vyombo vya habari, makundi ya wawekezaji na umoja wa wafanyabiashara wa sekta mbali mbali za kibiashara na kiuchumi, wanaharakati binafsi ndani na nje ya nchi yetu, wanamitandao kadhaa wa kijamii waliopo nchini na wasiokuwepo nchini na wengine wengi ambao siwezi kuwataja wote hapa.

Nchi nyingi duniani zimeimarisha mahusiano na umoja wa kitaifa kupitia janga hili. Msingi mkubwa ukiwa ni kuweka tofauti zao zozote pembeni, kisha kushikamana kwa nia moja. Mfano mmojawapo wa kipekee katika hili ni nchini Syria.

Hapa kwetu Tanzania, umoja wetu wa kitaifa unaelekea kuparaganyika zaidi kwa namna Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ilivyolipokea na inavyoratibu mapambano dhidi ya janga hili.

Kwa msingi huu, sasa tunaamini pasipo shaka kuwa njia bora zaidi ya kuisaidia Serikali na hatimaye wananchi ni kutokukaa kimya. Tunapotoa ushirikiano kwa kusema ndani ya vikao, Serikali haionyeshi kujali vya kutosha na inapunguza kasi ya mapambano katika vita hii.

Sasa tumeamua kuisaidia zaidi serikali kwa kuanika kwa uwazi maeneo mbalimbali ambayo tunaamini ikiyafanyia kazi itaweza kudhibiti kwa kiwango kikubwa janga hili.

Aidha, tunawasihi wananchi wote sasa wajifunze zaidi kupaza sauti zao katika kutetea uhai wao. Kila mmoja apige kelele kwani ukimya na upole wa Watanzania ndiyo unaowapa CCM na Serikali yao jeuri ya kupuuza maoni yao.

Madaraka na mamlaka yao yatambue wakati wote kuwa Mamlaka Kuu na ya mwisho hapa Tanzania ni Umma wa Watanzania wenyewe.

Sisi kama Chama Kikuu cha Upinzani hatuoni Serikali ikipokea na kutambua ushauri wetu. Tunaamini hali hii iko vilevile kwa vyama vingine na makundi mengine yaliyo nje ya CCM Serikali yake. Nina vielelezo kadhaa, kwa nini tunaamini hivyo.

Hapa nitafafanua kwa kifupi kwa nini Serikali ya Rais Magufuli na Chama Cha Mapinduzikwa pamoja vinaliingiza Taifa kwenye maafa makubwa sasa hivi na zaidi siku zijazo:

1. Kushindwa kabisa kwa Bunge kuisimamia Serikali katika kupambana na Janga la Corona:

Ibara ya 63.2 ya Katiba ya Nchi toleo la 1977 linatamka ifuatavyo: “… Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii”. … mwisho wa kunukuu.

Janga la Corona ni jambo kubwa linalotingisha binadamu duniani kote kuliko janga lolote katika miaka ya karibuni na likiwa na athari kubwa za kila aina. (The most severe global pandemic in modern time with devastating impacts on all spheres of life).

Kwa ukubwa wa janga hili, ungetegemea Bunge makini hadi hatua ya sasa, lingekuwa limeshaiamuru Serikali kuleta taarifa rasmi Bungeni ili kuwapa Wabunge, kwa niaba ya wananchi fursa ya kupata taarifa rasmi ya serikali, kuijadili na kuishauri na au kuielekeza hatua jumuishi za kuchukua.

Katika mazingira ya kutatanisha na kushangaza, Bunge halijatekeleza wajibu huu licha ya kuwepo maombi mara kadhaa toka kwa wabunge hususan wa upinzani kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji Bunge, kupitia hotuba mbalimbali za Wasemaji wa Kambi Rasmi wa Upinzani Bungeni, michango yao kuzungumza Bungeni au kupitia “Miongozo ya Spika”.

Rai hii ya upinzani, nimeifikisha binafsi kwenye vikao vyote mahsusi vya Kamati za Kiuongozi za Kibunge, bila kupewa kipaumbele chochote. Hii ni pamoja na Kamati ya Uongozi, Kamati ya Bajeti na hata Tume ya Utumishi wa Bunge.

Majibu mepesi ya Uongozi wa Bunge na Serikali siku zote yamekuwa ni kwamba, Serikali imeunda timu inayochambua na ikikamilisha itaiwasilisha Bungeni.

Watanzania wanaendelea kufa na kuumia kwa njia mbalimbali wakisubiri “wataalam wa Serikali” wakitafiti kinachojulikana (researching the obvious)!

USHAURI:
Bunge liitake Serikali kuleta taarifa rasmi na ya kina ya hali ya maambukizi ya Corona nchini, ijadiliwe na kuwekewa maazimio ya Bunge kwa niaba ya Wananchi katika kipindi cha siku zisizozidi 7.

2. Bunge kuendelea na mkutano wa bajeti katika mazingira ya kawaida bila kuzingatia athari kubwa za kiuchumi nchini na duniani kutokana na Janga la Corona.

Bunge linaendelea Dodoma kujadili na kupitisha makadirio ya
mapato na matumizi ya wizara na idara mbalimbali za Serikali kwa mwaka ujao wa fedha (2020/2021). Katika wajibu huu, Bunge pia huchambua utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka unaokwisha, (2019/2020).

Bunge linaendelea na wajibu huu kama vile hakuna athari zozote zinazoweza kuathiri mapato ya Serikali na hivyo kulazimika kuathiri matumizi yake.

Jambo hili likiendelea kama ilivyo, inaondoa maana yoyote ya kimantiki ya Bunge kuidhinisha mapato na matumizi ya Serikali. Ikumbukwe mzunguko wa bajeti ya Serikali (government budget circle) huanza tangu mwezi Oktoba, kila mwaka na kuhitimishwa June 30 ya mwaka unaofuata.

Janga la Corona limezuka katikati ya mchakato wa mzunguko wa bajeti lakini serikali na Uongozi wa Bunge haujaona maana yoyote ya “ku-adjust” maoteo na makisio kukabiliana na ukweli kuhusu Janga la Corona.

USHAURI:
• Serikali iwasilishe kwenye Bunge katika misingi ya dharura (ambapo utaratibu wa kawaida hautatumika) taarifa rasmi ya athari za kiuchumi za Janga la Corona kipekee kuhusu hali halisi ya maoteo ya mapato ya Serikali.
• Serikali ifanye marekebisho makubwa ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021 kufuatana na uhalisia utakaodhihirika, ndipo Mkutano wa Bajeti uweze kuendelea kwa maoteo hayo mapya na siyo kuendelea na maoteo na makisio yanayojadiliwa sasa kwani hayatekelezeki na ni kuendelea kupoteza fedha za wananchi.

3. Serikali kukosa hadi leo bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kupambana na Corona.

Corona si janga la nchi tu bali ni janga la dunia nzima. Nchi yeyote inayopuuza ukweli huu hujiingiza katika matatizo makubwa ndani ya nchi yenyewe na hata mbele ya Jamii ya Kimataifa.

Kielelezo cha kwanza cha utashi wa kisiasa na kiutawala wa nchi yeyote makini, ni kwanza kutambua na kukiri jambo husika kuwa janga; na pili kuishirikisha jamii husika nayo kulitambua janga; na tatu kuweka miundombinu wezeshi yenye mikakati shirikishi na yenye bajeti mahsusi.

Hadi leo, siyo Bunge wala Watanzania wanaelewa Serikali ina mkakati gani na imetenga bajeti kiasi gani kupambana na Corona. Awali, tulisikia Rais akibadilisha bajeti iliyotengwa kwa ajili ya mbio za Mwenge (Shs Bilioni 1) na baadaye tena tukasikia fungu lililotengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano (Shs Milioni 500) nazo zikibadilishiwa matumizi na kupelekwa kwenye bajeti isiyojulikana ya Corona.

Bajeti ya Corona imekuwa siri kubwa ya Serikali hadi sasa. Kwa uzito wa janga lenyewe, Serikali ingeweza kulishughulikia suala hili kupitia Kifungu namba 140 (1) na (2) cha Katiba ya Nchi kinachohusu Mfuko wa Matumizi ya Dharura. Kifungu hiki hata hivyo, kimesisitiza ushirikishwaji wa Bunge katika kubariki matumizi hayo ya dharura. Jambo hili bado halijafanyika.

Sheria ya Bajeti (Budget Act, Cap 439 R.E 2015), kupitia kifungu namba 34 (1) nayo inaipa Serikali nafasi ya kubadilisha matumizi yaliyoidhinishwa na Bunge kwa muda maalum yanapotokea majanga makubwa ambayo hayakutegemewa (major natural disaster or other significant unforeseen event).

Vifungu cha 34 (3), 35 – 39 vya sheria hii ya budget kinamtaka Waziri wa Fedha kutoa taarifa za matumizi hayo na kupata kibali cha Bunge. Jambo hili nalo hadi leo halijafanyika na ni dhahiri Serikali inaendelea kutumia fedha toka Mfuko Mkuu wa Hazina (Consolidated Fund) kupitia mfuko huu wa dharura (Contingency Fund) bila kulishirikisha Bunge.

Hadi leo Serikali haijaleta Bungeni “Supplimentary Budget’ kama inavyoelekezwa na kifungu cha 43 cha sheria hii.

USHAURI:

• Serikali isiendelee kufanya janga hili ni la siri. Itambue linahitaji uwazi, ukweli na ushirikishwaji.
• Janga la Corona linahitaji bajeti mahsusi katika mwaka huu wa fedha unaoendelea (2019/2020) ambapo ibara ya 140 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu.
• Kwa kutumia vifungu vya Sheria ya Bajeti namba 34 hadi 39 Serikali ifanye, panapostahili, mabadiliko ya matumizi yaliyokuwa yameidhinishwa na Bunge na kupeleka mafungu zaidi ya dharura kwenye bajeti maalum ya kupambana na Corona.

4. Serikali kubeza ushauri wa tahadhari ya awali (Initial Rapid Response) na kutokuona umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye kupima maambukizi kama mkakati wa kupunguza maambukizi.

Baada ya Shirika la WHO kutangaza Corona kama Janga la Kimataifa, nchi kadhaa zilichukua hatua za haraka za kuzuia maambukizi. Nchi hizo kwa kiwango kikubwa zilitayarisha wananchi wao sambamba na kuweka miundombinu sahihi katika hatua za awali.

Serikali yetu ilibeza janga hili na hata Rais kuliita “kaugonjwa kadogo” kanakoweza kumalizwa na “imani za dini kwa kumtumainia Mungu”, badala ya Sayansi na maelekezo ya WHO.

Maelekezo mahsusi ya Rais, mara nyingi yamejikita kwenye “kuomba Mungu” kama njia ya uhakika zaidi ya kupambana na janga hili. Kama Kiongozi Mkuu wa Nchi, amebeza mapendekezo ya kitaalam na bila soni ameendelea kutamka bayana kuruhusu mikusanyiko ya ibada.

USHAURI:

• Serikali sasa ifanye mpango wa haraka wa kupima ili waathirika waweze kutengwa kuzuia maambukizi zaidi.
• Serikali isione haya kuwasiliana na Serikali ya Senegal kuona uwezekano wa kutumia utaalam wao ambao umethibitishwa na WHO ambao ni wa gharama nafuu.
• Serikali itumie zaidi ya mashine 200 zijulikanazo kama “Gene X-pert” zilizotengenezwa na Kampuni ya CEPHEID ya Ufaransa zilizosambaa nchi nzima na zilizoingizwa nchini kwa ajili ya kupima TB na HIV. Iagize haraka “catridge” za kupima COVID 19 kama ilivyoshauriwa na mashirika kadhaa ya kimataifa.

5. Serikali “kuhodhi” bila kushirikisha makundi mengine kwa ukamilifu mapambano dhidi ya vita hii.

Ushirikishwaji mkubwa wa Umma katika vita hii imekuwa kwa kupokea michango na misaada zaidi. Waziri Mkuu, mara kadhaa ameomba Watanzania wawaamini lakini wao (Serikali) hawaoni ulazima wa kuwaamini wasio Serikalini au kwenye chama chao cha CCM (kama kweli nao wanajua kinachoendelea).

Usiri mkubwa na mkakati wa Serikali wa kuhodhi vita hii, umepelekea ombwe kubwa la ufahamu na uelewa wa kinachoendelea Serikalini. Ombwe hili limezaa malalamiko na hisia nyingi hasi miongoni mwa jamii na Serikali inastahili kubeba lawama hizi.

USHAURI:
• Serikali iunde National COVID 19 Task Force. Ishirikishe wadau wengine nje ya Serikali na iwepo kwa ngazi zote kuanzia Taifa, Mikoa (Regional COVID 19 Task Force), Wilaya (District COVID 19 Task Force)….na kuendelea hadi ngazi ya Kata, Vijiji/ Mitaa/Shehia.
• Task Force za kila ngazi zijumuishe wadau wote muhimu katika ngazi zao na ziongozwe na Viongozi wa Serikali.
• Wadau waruhusiwe kubadilisha kiongozi katika ngazi husika pale wadau watakapoona vinginevyo.
• COVID 19 Relief Fund iliyoundwa ngazi ya Taifa iundwe ngazi zote na zisimamiwe na Task Forces katika ngazi zao.
• Covid Task Forces zote ziwe na hotline ambapo wananchi wanaweza kutoa taarifa za matukio yanayohusu Janga la Corona wakati wote.

6. Serikali kukosa mkakati wa ndani wa wazi wa kukabiliana na anguko kubwa la uchumi.

Kwa kipindi cha miezi isiyozidi minne tangu Janga za Corona kuanza, uchumi wa dunia umeanguka kwa kiasi ambacho hakijapata kutokea tangu enzi za “Great World Economic Depression”, anguko kubwa la uchumi lililoikumba dunia kuanzia mwaka 1929 – 1939. Hii ni miaka 90 iliyopita.

Anguko la uchumi wa dunia haliwezi kuuacha uchumi wa Tanzania ukiwa imara hasa ukizingatia uchumi wetu ulivyo tegemezi.

Pamoja na serikali kusisitiza kutochukua hatua mahsusi za “ku-lock down” (Full or partial lockdown); kuwepo kwa taharuki ya dunia inayoambatana na hofu kubwa ambayo ni dhahiri na siyo bandia (kama anavyodai Rais wetu); sekta muhimu katika uchumi wetu tayari zimeathirika sana na zitakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi, makampuni yanayohusika na sekta hizo na wananchi walioajiriwa au washiriki katika mnyororo wa thamani (value chain) katika sekta hizo.

Hatuna “lock down” inayodhibitiwa bali tuna “slowdown” isiyodhibitiwa. Wananchi na makampuni hayawezi kuisubiri Serikali inayofanya utafiki kwenye mambo yaliyo wazi wakati tayari vifo viko mlangoni na miongoni mwetu!!

Sekta zilizoathirika sana ni pamoja na utalii, kilimo, biashara ya anga (aviation), sekta ya madini ya vito, biashara ya uuzaji nje na uagizaji nje, sekta ya fedha na sekta ya elimu.

Sekta ya utalii ni ya pili kwa ajira baada ya sekta ya kilimo. Huchangia robo (25%) ya fedha za kigeni katika taifa na asilimia 18 ya pato la Taifa. Sekta hii imekwama kwa zaidi ya asilimia 98% na hadi sasa Serikali iko kimya!

Hoteli zote na makampuni ya utalii yamefunga kabisa biashara. Watumishi wengi wamepoteza ajira. Sekta hii haitegemewi kuamka chini ya miaka miwili ijayo tena kama mataifa yanayotuletea watalii watarejesha imani kwa nchi yetu kwa namna tulivyochukulia kimzaha mapambano dhidi ya Janga la Corona. Bado serikali ambayo ni mnufaika namba moja, haijaona jambo hili ni janga la taifa.

Pamoja na ushauri wa wadau wengi kuhusu serikali kuja na mikakati ya sera za kodi na sera za kifedha kupunguza makali ya anguko la uchumi kwa makampuni na wananchi, serikali bado iko sirini ikifanya utafiti.

USHAURI:
• Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta Binafsi na Taasisi nyingine itengeneze stimulus package maalum kwa ajili ya kukabiliana na athari za kiuchumi na ajira yatokanayo na janga hili.

7. Serikali kuweka usiri mkubwa wa taarifa za hali halisi ya maambukizi na vifo vitokanavyo na ugonjwa huu kwa wananchi.

Kumekuwepo mkanganyiko mkubwa katika utoaji wa taarifa sahihi zinazohusu maambukizi na vifo vya janga hili. Serikali na zaidi Rais Joseph Pombe Magufuli yuko katika hali ya kutokubali hali halisi (state of denial). Hali hii ilijidhihirisha Rais alipokutana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, akiwa nyumbani kwake Chato, Mkoani Geita.

Mambo kadhaa yasiyo ya kawaida yalijitokeza:
• Rais aliongea na Vyombo vya ulinzi na Usalama mambo yanayohusu sayansi na utabibu.
• Rais aliwaondoa “kazini” wataalam wawili muhimu na wazoefu katika Wizara ya Afya. Hawa ni Katibu Mkuu wa Wizara, Daktari wa Binadamu Zainab Chaula (ambaye amehamishiwa Wizara isiyohitaji mtabibu) na Prof. Bakari, Mganga Mkuu wa Serikali (ambaye tunaambiwa amestaafu). Pamoja na Rais kuwa na mamlaka hayo, busara zetu ndogo, zinatufundisha kuwa si jambo la kawaida kubadilisha ‘majenerali’ katikati ya vita. Aidha, mataifa mengine yanawaita kazini wastaafu wake wa fani ya utabibu kukabiliana na tishio hili sisi mkuu wetu anastaafisha!!
• Rais alipingana hadharani na takwimu zinazotolewa na wasaidizi wake walio mstari wa mbele katika vita hii. Hawa ni pamoja na Waziri Mkuu, Waziri wa Afya na Naibu wake. Pia Watendaji Wakuu wa Wizara, Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali walioondolewa.
• Rais alionekana kukwazika na ongezeko la idadi ya maambukizi na vifo vinavyoripotiwa ambayo wasaidizi wake hao walishaitangazia dunia kuwa walioambukizwa wamefikia 284. Alitamani kusikia wengi waliopona akidai yeye anajua waliopona ni 100 ilihali wasaidizi wake wanasema ni 11!! Hii ilikuwa tarehe 22 Aprili 2020. Hadi leo, kabla ya taarifa ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa iliyotolewa muda mfupi uliopita, kulikuwa hakujaripotiwa taarifa nyingine kuhusu ongezeko la maambukizi wala vifo bali taarifa za waliopona zaidi.
• Rais alionekana kuendelea kupuuza maelekezo ya wataalam ikiwemo fumigation, karantini, uvaaji wa barakoa na hata uzoefu wa mataifa mengine katika kukabiliana na janga hili.
• Rais aliendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda uchumi kama kipaumbele chake namba moja kuliko kupigania uhai wa watu wake.
• Rais kuonyesha nia ya kutumia majeshi kudhibiti hisia za Raia pale wanapohoji au kudadasi hali halisi ya Janga la Corona hususan mitandaoni.

Wakati Serikali ikiendelea kuweka usiri mkubwa wa maambukizi na vifo, nchini tunashuhudia ongezeko la vifo vya watu wengi, tena wengine wakizikwa na serikali kimya kimya, bila serikali kuweka wazi kuwa ni vifo vya Corona au kitu gani!

Aidha taarifa za kusambaa zaidi kwa ugonjwa huu ghafla zimekatika bila maelekezo ya kutosha toka serikalini, jambo linalozua taharuki kubwa kwa wananchi.

USHAURI:
• Rais wetu na Serikali yake yote wasione aibu kutoa kwa umma na Dunia taarifa za ukweli kuhusiana na maafa haya.
• Kuendelea kuficha kama inavyofanyika sasa kunasababisha taharuki kubwa kwa wananchi.
• Usiri katika janga hili unaondoa ufahamu (awareness) na hivyo kuongeza kwa kasi ongezeko la maambukizi.
• Viongozi wa Serikali watambue kuwa usiri unaosababisha vifo vya halaiki chini ya mamlaka yao hutafsiriwa kama ushiriki wa mauaji na ni kosa la uhalifu dhidi ya binadamu katika Mahakama za Kimataifa.
• Wananchi wanastahili kupata taarifa za kina kama ilivyoelekezwa na Katiba ya Nchi.

CHADEMA TUTAFANYA NINI KATIKA HILI
• Huku tukitambua umuhimu wa taarifa; na tena tukitambua usiri mkubwa wa Serikali wakati huu; na tena tukijua ukweli na uwazi utaliweka Taifa katika kuelewa na hivyo kuchukua tahadhari stahiki, tutafanya yafuatayo:
I. Tunatangaza kuunda CHADEMA COVID 19 ADVISORY TASK FORCE itakayoongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Taifa.
II. Namba ya mawasiliano (Hotline) itakuwa +255-744-44-69-69 ambayo itakuwa namba ya WhatsApp tu.
III. Taarifa mbalimbali za picha na maandishi zinaweza kutumwa kwenye namba hiyo.
IV. Kamati kama hizi zitaundwa na kuongozwa na Makatibu wa Chama katika ngazi zote hadi kwenye misingi.
V. Wajibu wa msingi wa Kamati ni kukusanya taarifa za vifo vyote katika maeneo yao ya uongozi kwa utaratibu utakaotolewa mwongozo na Katibu Mkuu, na kuziwasilisha kwa ngazi ya juu yake ya uongozi na kwa mtiririko huo huo hadi ngazi ya Taifa kwa Katibu Mkuu.
VI. Kila kiongozi katika ngazi zote za chama, taifa hadi msingi, watambue uhai wa Watanzania si jambo la masihara na wawe tayari kuulinda kadiri iwezekanavyo.
VII. Wanachadema wote tukatae kuficha ukweli kuhusu ugonjwa ili tuepushe vifo visivyokuwa vya lazima.

8. Serikali kukosa mkakati wa makusudi wa kulinda Watumishi wa Kada ya Afya wakiwemo madaktari na wauguzi dhidi ya maambukizi.

Katika vita dhidi ya Corona, askari wetu walio mstari wa mbele ni Wataalam wa Kada ya Afya inayojumuisha, madaktari, wauguzi, lab technicians na wengine wengi. Hawa wanafanya kazi ngumu ya kuokoa maisha ya watu wakati wao wenyewe wakihatarisha ya kwao.

Cha kusikitisha zaidi kwa sasa, hofu ni kubwa sana kwenye kada ya watumishi hao. Wengi hawana vifaa ya kujilinda (PPE), hali inayopelekea wauguzi na madaktari sasa kuwakimbia wagonjwa siyo wa COVID19 pekee, bali wote kwani si rahisi kuwatambua walioathirika kwa sababu hatuna mkakati wowote wa kuwapima na kuwatenga wale walioathirika.

USHAURI:

• Kasi ya maambukizi ilivyo kwa sasa, inahitaji kada hii ya wataalam nchi nzima ipatiwe vifaa/mavazi maalum ya kuwakinga na maambukizi wawapo katika huduma. Vifaa hivi hujulikana duniani kama PPE (Personal Protection Equipment).
• Vifaa hivi visitolewe kwa vituo vinavyohudumia Janga la Corona pekee bali vituo vyote vinavyotoa huduma ya afya nchi nzima, vikiwamo vya watu na taasisi binafsi. Hii ni kwa sababu kwa kiwango cha maambukizi yalivyo sasa, tofauti na pale mwanzoni; waathirika wamesambaa nchi nzima na wengi hawajitambui.
• Kadri iwezekanavyo, watumishi hawa wa afya hususan wale wanaoshughulika moja kwa moja na wagonjwa wa Corona, wapewe makazi maalum yaliyotengwa ili kutoa amani kwa familia zao hadi pale janga hili litakapopunguza kasi ya kusambaa.
• Serikali iajiri angalau kwa muda maalum wataalam wote wa afya ambao hawana ajira na waliostaafu wakiwemo wataalam wa “Epedemiology’ kusaidiana na waliopo.

9. Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar kutokusimama msitari wa mbele kuongoza mapambano. Serikali kukosa mkakati wa wazi wa kimahusiano kimataifa.

Janga la Corona linagusa kila nchi, jumuiya, taasisi, mashirika, wawekezaji, wafanyabiashara, wanasayansi na kila binadamu. Pamoja na nchi nyingi duniani kukumbwa na janga hili, pamekuwapo na juhudi kubwa za nchi mbali mbali kupitia Viongozi wao Wakuu kuweka mikakati ya mahusiano inayopelekea nchi hizo kusaidiwa kwa urahisi zaidi misaada ya vifaa tiba na hata fedha kupambana na janga hili ikiwemo kupoza athari za kuanguka kwa uchumi wa nchi zao.

Mahusiano bora ya kimataifa ni zao la kusikika kwa Viongozi Wakuu wa mataifa mbalimbali wakihamasisha vita dhidi ya janga hili ndani na nje ya mipaka ya nchi zao. Ujenzi wa mahusiano hayo si lazima yajengwe na mifumo rasmi ya kiserikali na kidiplomasia, bali hata kupitia kwa mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayofanya ushauri wa kimikakati (Strategic Lobbying).

USHAURI:

• Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar wajotokeze kuongoza vita hii kwenye msitari wa mbele.
• Serikali ione umuhimu wa kushirikiana na nchi nyingine za Jumuia ya Afrika ya Mashariki.
• Raisi J.P Magufuli atumie nafasi yake ya Mwenyekiti wa SADC kuongoza umoja wa nchi hizo kupambana na Janga la Corona na hivyo kuiweka Tanzania katika nafasi ya heshima mbele ya mataifa mengine.
• Serikali itafakari upya mahusiano yake na WHO kwani kuna malalamiko kutoka shirika hilo kuwa Tanzania haiko makini kushughulika na Janga la Corona. Hilo ni doa kubwa sana kwa nchi yetu huko tuendako.
• Serikali itumie fursa mbalimbali zilizopo kwa Rais kutoka na kauli za kujenga mahusiano bora na Mashirika Makuu ya Fedha duniani (IMF na World Bank) badala ya mambo haya kufanywa na wasaidizi wake.

10. RAI YA CHADEMA KWA TAIFA

• Kila Mtanzania mmoja mmoja awe hatua ya kwanza kutekeleza mbinu ya kujikinga na maambukizi haya.
• Kwa wanaohisi kuathirika, wakati bado wanatafuta suluhisho la kitabibu, wachukue tahadhari za mapema kuwalinda wenzao.
• Kila kaya, iwe hatua ya pili ya kujikinga na maambukizi. Kila Kiongozi wa Kaya awe mstari wa mbele kuhakikisha kaya yake inachukua tahadhari makini iwezekanavyo.
• Maelekezo ya Wataalam wa Afya yazingatiwe kwa umakini mkubwa.

Imetolewa Jumatano, 29 Aprili 2020

Freeman Aikaeli Mbowe

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa
Kiongozi wa Upinzani Bungeni
Mbunge wa Hai

Share Button