TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

NEC IJINASUE KATIKA TUHUMA ZA KUHARIBU NA KUVURUGA UCHAGUZI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiwa sehemu ya wadau wa uchaguzi nchini kinaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza hadharani kwa umma ratiba ya kuanza kuboreshwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) kama Katiba na Sheria za Nchi, zinavyoelekeza.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 74(6) Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inayo mamlaka ya kuratibu na kusimamia uandikishaji wa wapiga kwenye DKWK kwenye Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Madiwani kwa Tanzania Bara. Aidha, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, kifungu cha 15(5) na kifungu cha 21(5) inaiamuru NEC kufanya uboreshaji wa DKWK mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na unaofuata. Hivyo basi ni wazi kuwa kitendo cha NEC kutoboresha DKWK tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ni kukiuka Katiba na Sheria za Nchi.

Kupitia taarifa hii, kwa mara nyingine tena, tunaitaka NEC itoe ratiba ya uandikishaji wa DKWK kwa nchi nzima, kwani mbali ya kutekeleza matakwa ya sheria, ratiba hiyo pia ni sehemu ya mwongozo kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi kujipanga na kufanya maandalizi ya kushiriki uandikishaji, ambapo ni pamoja na wapiga kura, vyama vya siasa (kuhamasisha wananchi na kuweka mawakala), na waangalizi wa zoezi hilo.

Sambamba na hilo, kupitia taarifa hii, tunaitaka NEC kueleza kwa umma kwanini imetoa muda wa siku mbili kwa ajili watu wenye sifa kutuma maombi ya nafasi za kazi za muda kwa ajili ya uboreshaji wa DKWK, huku siku ya kazi ikiwa ni moja pekee. Itakumbukwa kuwa tangazo la NEC lilitolewa Alhamis Mei 30 na mwisho wa kuwasilisha maombi ulikuwa ni kabla ya Jumapili, Juni 2, 2019. Ni wazi siku hizo hazitoshi kwa zoezi hilo muhimu katika mchakato wa uchaguzi, hivyo tunaitaka NEC kuongeza muda wa kutosha watu kutuma maombi hayo na kuwapata watu wenye sifa stahiki.

Hali hiyo ya NEC kukiuka sheria za nchi kwa kutoboresha DKWK na kutoa muda mfinyu wa kuwapata watu wenye weledi wa kutosha kufanya kazi ya ukarani wa kusimamia uandikishaji ni dalili zinazotosha kutilia shaka umakini na utayari wa NEC katika kusimamia uchaguzi (huru na haki) mkuu wa mwaka 2020. Tunaitaka NEC ifanye kazi zake kwa kuzingatia sheria, ikiwemo kutangaza ratiba ya kuandikisha wapiga kura na kuongeza muda wa kuwapata makarani, ili kujinasua katika tuhuma nzito za kuharibu na kuvuruga uchaguzi nchini. Ni muhimu itambue kuwa uchaguzi si tukio la siku moja ya kupiga kura, bali ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali ambazo zote zinapaswa kuzingatia haki za wapiga kura na hasipaswi kutiliwa shaka hata mara moja.

Imetolewa leo Jumatatu, Juni 3, 2019 na;

Tumaini Makene

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Share Button