Kumekuwa na taarifa zinazosambaa katika njia mbalimbali za upashanaji habari mitandaoni na baadae kwenye vyombo vya habari tangu asubuhi ya leo kuhusu kile kinachoonekana kuwa ni sintofahamu kubwa inayoendelea katika Bunge la Afrika (PAP) ambako taarifa zimedai kuwa Rais wa PAP, Roger Nkodo Dang anatakiwa kujadiliwa na Bunge hilo kutokana na tuhuma nzito zinazomkabili ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, unyanyasaji wa kingono, upendeleo na unyanyasaji kwa wafanyakazi wa Ofisi za Makao Makuu ya Bunge hilo, nchini Afrika Kusini.

Taarifa hizo za maneno zilizokuwa zikisambaa zilipewa nguvu na video fupi iliyorekodiwa ikimuonesha Makamu wa Rais wa PAP, Stepehen Maselle (ambaye ni mmoja wa wawakilishi wanne katika PAP) akizungumza wakati akiongoza mojawapo ya vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea nchini Afrika Kusini kwa sasa, ambapo amesikika (tafsiri yetu ya Kiswahili) akimlalamikia Rais wa PAP kuwa amemwandikia barua Spika wa Bunge la Tanzania ili amrejeshe Stephen Masele nchini (recalling) ili ikiwa ni namna ya Rais huyo kupambana kuzuia agenda au taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza tuhuma zake isisomwe, kujadiliwa au kufanyiwa kazi na Bunge hilo. Katika video hiyo Mbunge huyo amesikika akisema anayo ruhusa kutoka kwa Waziri Mkuu (Serikalini) hivyo hataondoka nchini Afrika Kusini kama ambavyo Rais huyo wa PAP anataka iwe, katikati ya mapambano yake ya kujisafisha na tuhuma hizo nzito zinazomkabili.

Kabla Watanzania hawajaelewa hasa kinachoendelea, kutokana na mkanganyiko huo ambao umeanza kushika kasi kwenye vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa, Spika wa Bunge Ndugu Job Ndugai ametoa taarifa ya Bunge akithibitisha maneno yaliyokuwa yakisambaa mitandaoni kuwa Bunge limemuagiza Stephen Maselle arejee nyumbani haraka kuja kujibu tuhuma za ukosefu wa maadili zinazomkabili mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge pamoja na Kamati ya Maadili ya Chama chake.

Katikati ya mkanganyiko huu, CHADEMA inapenda kuweka msimamo wake wazi kuwa jina la nchi yetu Tanzania lisitumike vibaya wala kuwekewa taswira hasi na kuendelea kuharibu sura yetu kidiplomasia na katika mahusiano ya kimataifa.

Tunasema hivyo tukiwa na taarifa za uhakika kuwa PAP ililazimika kuunda Kamati Maalum kuchunguza tuhuma hizo nzito zinazomkabili Rais wake, Roger Nkodo Dang, za unyanyasi wa kingono kwa watumishi wa kike walioko Makao Makuu ya PAP (imedaiwa takriban wanawake 10 wamejitokeza mbele ya kamati kuthibitisha walivyonyanyaswa kingono bila ridhaa yao), matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo dani ya bunge hilo na unyanyasaji kwa watumishi wa ofisi hiyo hali iliyosababisha kuwepo kwa mgomo wa watumishi kwa takriban wiki nzima.

Taarifa tulizozipata kutoka ndani ya Bunge hilo zimedai kuwa Rais Roger Nkodo Dang anatumia njia mbalimbali kupambana kujisafisha na tuhuma hizo kwa sababu mbali ya kupoteza nafasi yake hiyo kwenye Bunge la PAP, iwapo zikithibitika kuwa ni kweli, pia zitamuondolea kinga za kidiplomasia alizonazo, huku ikijulikana wazi kuwa tuhuma hizo zinazomkabili ni mojawapo ya makosa makubwa ya kijinai yanayochukuliwa kwa uzito mkubwa nchini Afrika Kusini.

Katika mazingira hayo, kitendo cha Bunge kumrejesha nyumbani kwa haraka Makamu wa Rais wa PAP, Stephen Masele ambaye kiutaratibu ndiye aliyetakiwa kuongoza vikao vya Bunge hilo vinapojadili taarifa ya Kamati Maalum kuhusu tuhuma za Rais na kusimamia utekelezaji wa maazimio, inaibua shaka kubwa na kujenga taswira hasi kwa nchi yetu kuwa inatumika au inataka kutumika kumuokoa Rais Roger Nkodo Dang dhidi ya tuhuma hizo au haitaki kuonekana kuwa imesimamia na kuongoza taratibu zinazotakiwa katika suala linalomsibu na pengine kitakachofuatia.

Hivyo basi ili kuiweka nchi yetu katika mahusiano mazuri ya kimataifa na kuendeleza sifa yetu iliyojengwa kwa miaka mingi huko nyuma kuwa Tanzania inasimamia misingi na taratibu na kuondoa kadhia itakayoijengea nchi yetu picha mbaya, si ndani ya nchi pekee mbali kimataifa pia, tunalitaka Bunge (lililomrejesha nyumbani Stephen Masele) na Serikali ya Tanzania ambayo imedaiwa kumwagiza Stephen Masele aendelee kubaki huko hadi amalize majukumu yake, kutoa kauli ya msimamo wetu Tanzania kuhusu tuhuma zinazomkabili Rais wa PAP. Je ni kweli tunaunga mkono unyanyasaji wa kingono? Je tunaunga mkono matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo rushwa? Je tunaunga mkono unyanyasaji? Je tunaunga mkono upendeleo katika taasisi hiyo ya kimataifa?

Ni msimamo huo pekee utaweza kuiokoa Tanzania katika jambo hilo ambalo limeanza kuchukua mkondo mbaya kuwa nchi yetu inatumika kulinda tuhuma za uhalifu wa kijinai.

Aidha, kwa sababu Spika wa Bunge ameshalizungumzia na kulitolea taarifa suala hilo hatua iliyomaliza utata wa iwapo taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni zilikuwa za kweli, tunalitaka Bunge kuweka wazi tuhuma zinazomkabili Mbunge Stephen Masele zilizosababisha arejeshwe nchini na uwakilishi wake (wa nchi) katika taasisi hiyo ya kimataifa kusitishwa.

Halikadhalika, CHADEMA inaitaka mihimili ya Serikali na Bunge kutoka hadharani na kutoa kauli kuueleza umma juu ya madai kuwa kuna hali ya mgongano wa kauli, misimamo na maamuzi baina ya mihimili hiyo miwili juu ya suala hilo, kiasi ambacho kimeanza kuleta athari katika uwakilishi wa nchi yetu kwenye PAP. Kauli ya mihimili hiyo itawasaidia wawakilishi watatu wa Tanzania waliosalia kwenye PAP kujua misingi ya hoja zao na masuala wanayotakiwa kusimamia katika mtanziko huu uliopo.

*Imetolewa leo Alhamis, Mei 16, 2019 na;*

*Tumaini Makene*
*Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano*
*CHADEMA*

Share Button