TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

KUHUSU:

BAADA YA HUKUMU YA MAHAKAMA KUU, MASUALA SABA YA MUHIMU; UCHAGUZI HURU NA HAKI NCHINI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepanua wigo wa mjadala wa uhitaji wa taasisi na mifumo itakayohakikisha nchi inafanya chaguzi huru na haki kwa kuitaka Serikali kufanyia kazi masuala 7 muhimu, wakati huu inapojiandaa kutekeleza amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo imefuta vifungu 7(1) na 7(3), vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi namba 5 ya mwaka 1985, vilivyokuwa vikiwapatia mamlaka wakurugenzi wa halmashauri nchini kusimamia uchaguzi.

Aidha, CHADEMA kimetoa rai kwa wadau mbalimbali wa demokrasia na utawala bora ndani na nje ya nchi kupigania na kusaidia kwa kila njia inayowezekana kutekelezwa kwa masuala hayo 7, kwa sababu mfumo wa uchaguzi huru na haki ni mojawapo ya sifa kuu za demokrasia duniani zinazodhihirisha mamlaka ya wananchi katika kuamua namna wanavyotaka kujitawala na kuongozwa.

Pia, taasisi imara na mifumo thabiti ya chaguzi huru na haki, inaondoa uwezekano wa nchi kutumbukia katika machafuko kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huku pia ikidhibiti mianya ya kuchaguliwa na kuwekwa madarakani mamlaka za kidikteta zenye kujali na kusimamia maslahi ya wachache badala ya maslahi ya taifa na matakwa ya wananchi.

 Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo Makao Makuu ya CHADEMA, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uenezi, Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema ameyataja masuala hayo 7 ambayo CHADEMA kinaamini ni sehemu muhimu ya mjadala wa muda mrefu nchini kuhusu hitaji la chaguzi huru na za haki, kuwa ni pamoja na;

1.     Tume Huru ya Uchaguzi (Tanzania Independent Electoral Commission-TIEC)

2.     Matokeo ya uchaguzi wa rais kupingwa mahakamani

3.     Haki ya mgombea kukata rufaa (na kupata haki yake ya kugombea) anapokuwa amenyimwa fomu, fomu zake kukataliwa kupokelewa au kutoteuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi.

4.     Mfumo usiruhusu mgombea kupita bila (kupingwa) kupigiwa kura.

5. Mfuko Maalum wa Fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za TIEC kusimamia uchaguzi.

6. Maamuzi ya Tume Huru ya Uchaguzi kuweza kupingwa mahakamani.

7. Kuwepo kwa mgombea binafsi.

CHADEMA inaweka bayana kuwa mapendekezo hayo ni kwa ajili ya maslahi ya nchi hasa Watanzania wanapojiandaa kuelekea kwenye chaguzi mbili muhimu, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2019) na Uchaguzi Mkuu (Rais, Wabunge na Madiwani-2020), ambapo wapiga kura wanahitaji kuhakikishiwa kuwa karatasi za kura sio tu ziko salama, bali hazitaangaliwa kama karatasi zingine za kawaida.

“CHADEMA tunapendekeza iundwe Tume Huru ya Uchaguzi kwa maana ya TIEC, Tanzania Independent Electoral Commission) ambayo itawekewa utaratibu mpya wa uteuzi kuwapata wajumbe wake, mathalani katika nchi za Kenya, South Africa, Malawi au Ghana watu hao wanapatikana kwa kutuma maombi ya kazi na kufanyiwa vetting (uchambuzi) na mamlaka husika kabla ya uteuzi. Uteuzi uwe huru usiwe chini ya mtu mmoja ambaye naye anakuwa na maslahi binafsi au ya chama chake wakati wa uchaguzi. Tunataka wajumbe wa Tume wawe na uhakika wa usalama wanapotimiza majukumu yao. Muhula wao kazini ujulikane na ulindwe. Masharti yao ya kazi yajulikane. Mnakumbuka wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, kuna watumishi waliondolewa kazini katikati ya uchaguzi kinyume cha utaratibu.”

“Tunataka TIEC hiyo iwe na mfuko wake maalum kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake badala ya kupiga magoti kuombaomba Serikali Kuu. Hii inapunguza uhuru wa Tume kwa sababu inaomba fedha kwa watu ambao inatakiwa kuwasimamia. Mfano mzuri ni huu wa sasa ambapo Tume ya Uchaguzi haijaandikisha daftari la wapiga kura, kinyume na maelekezo ya kisheria ambayo yanataka daftari liandikwe mara mbili. Hii ni kwa sababu tume haina mfuko wake wa fedha zake yenyewe, inasubiri hadi ipewe,” amesema Mrema.

Aidha, CHADEMA inasisitiza kuwa hakuna haja ya kuendelea kuwepo na zuio la kutoruhusu maamuzi ya Tume ya Uchaguzi kuhojiwa mahakamani, kwa sababu iwapo makamishna na watendaji wa Tume watajua kuwa tume inaweza kushtakiwa na kuhojiwa mahakamani watafanya maamuzi yao kwa kuzingatia haki ili wasifikishwe mahakamani. “Lakini pia kama tume ni huru kunakuwa na hofu gani ya kuzuia maamuzi yake kuhojiwa mahakamani? Maana yake basi hiyo tume isiyohojiwa mahakamani haiko huru.”

Huku ikitambua na kuunga mkono juhudi ambazo zimechukuliwa tayari na wadau wengine kwa kufungua kesi Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, ambayo tayari imesajiliwa kwa namba 018/2018, kwa ajili ya kupinga Ibara ya 41(7) inayozuia kuchunguza au kuhoji matokeo ya uchaguzi Mahakamani, kwa sababu ibara hiyo inakiuka Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, CHADEMA inaweka bayana kuwa ibara hiyo inapaswa kuondolewa ili mtu yeyote awe na haki ya kuhoji matokeo ya uchaguzi huo iwapo na ushahidi kuwa ulikuwa na makosa, kama inavyoruhusiwa kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Wabunge na Madiwani.

Kuhusu uwepo wa vifungu vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kifungu cha 45(2) na kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, vinavyoruhusu mgombea kupita bila kupingwa ikitokea ameteuliwa peke yake, CHADEMA inapendekeza kuwa ikitokea mazingira (yasiyokiuka sheria) kuwa mgombea ameteuliwa peke yake, asihesabiwe au asitangazwe kuwa ameshinda kwa kupita kupingwa bali wananchi wapate fursa na kutumia haki yao kwa kumpigia kura ya NDIYO au HAPANA. Mbali ya kuwapatia wananchi haki hiyo na kuona iwapo mgombea anaungwa mkono na wananchi, pia itaondoa uwezekano wa wagombea wengine kuenguliwa kwa hila kwa kunyimwa fomu, fomu zao kukataliwa au kutopokelewa au kutoteuliwa kwa makusudi, ili kumsaidia mgombea fulani apite bila kupingwa kama ambavyo imetokea katika chaguzi kadhaa hivi karibuni.

CHADEMA pia inataka kuwepo kwa mfumo wa kisheria utakaohakikisha utekelezwaji wa Ibara ya 21 ya Katiba ya Nchi, ili kuondokana na vikwazo wanavyowekewa baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali hasa wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa ama wakinyimwa fomu za kugombea, fomu zao kutopokelewa (wasimamizi kukataa au kujificha) au kuenguliwa wakati wa uteuzi huku haki yao ya kugombea ikiishia hapo, bila kuwa na haki ya kukataa rufaa, kama ilivyotokea wakati wa uchaguzi wa marudio Jimbo la Korogwe vijijini mwaka jana.

Katika hali ya kupinga ukiukwaji huo wa Katiba na haki za binadamu, aliyekuwa mgombea wa CHADEMA katika uchaguzi huo wa marudio Korogwe Vijijini, Bi. Aminata Suguti amefungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, kesi namba 7/2019 iliyoko mbele ya Jaji Mruma, tayari imetajwa mnamo tarehe 30 Aprili, mwaka huu na itaanza kusikilizwa Juni 4, mwaka huu. Upande wa mpeleka maombi unaiomba Mahakama kutoa amri kuwa iwapo mgombea hajateuliwa na msimamizi wa uchaguzi kwa sababu fomu zake hazikupokelewa, awe na haki ya kukata rufaa. Mahakama pia, iwe na mamlaka ya kumtangaza mgombea wa namna hiyo kuwa ni mgombea halali wa uchaguzi almuradi awe amepitia mchakato wa ndani wa chama chake.

Pia, CHADEMA imesema kuwa ni wakati mwafaka sasa kuwepo na Sheria inayoruhusu mgombea binafsi ili kutekeleza Katiba ya nchi, jambo ambalo pia litasaidia makundi mbalimbali katika jamii, ambayo hayahitaji kufungamana na itikadi za vyama vya siasa, kuwa na uwakilishi katika vyombo vya maamuzi.

CHADEMA imetoa wito kwa Serikali pamoja na Chama kilichoko madarakani kutokuwa na hofu ya kuweka mazingira yanayoweka misingi ya taasisi na mifumo imara kwa ajili ya chaguzi huru na haki, kwa sababu kama chama au serikali iliyoko madarakani imefanya kazi kama inavyotakiwa itachaguliwa katika mazingira hayo na itakuwa na uhalali zaidi wa kuongoza wananchi badala ya mfumo wa sasa ambao unatia walakini chaguzi zinazofanyika nchini, hivyo viongozi wengi wanaochaguliwa wanakuwa na uhalali wa kisheria lakini si uhalali wa kisiasa (kukubalika au kuungwa mkono na watu).

Imetolewa leo Jumapili, Mei 12, 2019 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Share Button