Mnamo Juni 18, mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume kabisa na Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Mwaka 2016, Kanuni ya 99 fasili ya 5, lilizuia kuwasilishwa mezani kwa Hotuba ya Bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019.

Halikadhalika lilizuia kusomwa kwa hotuba hiyo kinyume na Kanuni ya 99 fasili ya 9, huku pia uamuzi huo ukivunja Kanuni ya 14, inayotambua Ofisi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Kanuni ya 143 fasili ya 2 inayowatambua Wasemaji Wakuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hata katika itifaki ya ukaaji ndani ya ukumbi.

Zaidi ya kuvunja kanuni hizo za kudumu za bunge, uamuzi huo ulikuwa kinyume na maelekezo ya Spika wa Bunge, Ndugu Job Ndugai aliyoyatoa Aprili 19, mwaka huu, kwenda kwa Wanadhimu wa Bunge, kwa maana ya upande wa Serikali na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambapo aliwaelekeza kuwa taarifa za Kamati za Bunge au Kambi ya Upinzani ziwasilishwe bungeni, siku moja kabla ya kusomwa.

Mbali ya kusikitishwa na uamuzi huo, tumeshangazwa na kusikitishwa zaidi na majibu yaliyotolewa na Spika wa Bunge Ndugu Job Ndugai ndani ya bunge kuhusu kadhia hiyo, ambapo kwa mujibu wa vyombo vya habari mbalimbali, Spika Ndugai amenukuliwa akisema;

“…ninyi tumeanza Bunge la Bajeti Aprili hamna hotuba yoyote mliyotoa na sababu mliyotoa wanaowaandikieni hawapo, sasa kumbe mmepata wa kuwaandikia na hamna aibu kusema kuwa mmeandikiwa.”

“Badala ya ninyi kuandika halafu mnakuja kutusomea mmechangachanga hela mmepata wa kuwaandikieni, kweli kabisa, mmepata wa kuwaandikieni kurasa mia tatu.”
_
Tafsiri ya sehemu hiyo ya majibu ya Spika Ndugai inaonesha kuwa Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA au wabunge wetu, wanaandikiwa hotuba zao na kwamba hilo si jambo sahihi, kwani wanatakiwa kuandika wao wenyewe. Ndicho alichomaanisha Spika Ndugai.

Kwa uhakika, majibu hayo pamoja na uamuzi wa kuzuia hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti mbadala, ni mwendelezo wa vitendo vya ukiukwaji wa kanuni za bunge na udhalilishaji wa mamlaka ya bunge ambao unataka kufanywa kuwa ni sehemu ya utendaji wa bunge letu tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano.

Tuliamini kuwa kutokana na uzoefu wake mkubwa katika uendeshaji wa bunge letu na uelewa wake kuhusu utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola au hata mabunge ya nchi zingine, Spika Ndugai anajua kuwa wabunge ama mmoja mmoja au Kambi ya Upinzani Bungeni, Kamati za Bunge na Kambi ya Serikali Bungeni zinapaswa kufanya kazi kitaasisi.

Katika nchi zilizoendelea na zinazothamini unyeti wa wajibu wa Mhimili wa Bunge na umuhimu wa majukumu ya wabunge, mbunge mmoja si tu kwamba ana ofisi yake, bali pia anao watu kadhaa katika ofisi ambao wanapaswa kumsaidia majukumu mbalimbali, ikiwemo kufanya utafiti, kufanya uchambuzi, kuandaa na kuandika hotuba za michango mbalimbali anayowasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi wake.

Hata kwa uzoefu wake kwa Bunge la Tanzania ambalo amelitumikia kama Mbunge wa kawaida, Mwenyekiti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Naibu Spika na sasa Spika wa Bunge, akiongoza mhimili muhimu kabisa unaowakilisha wananchi, Spika Ndugai anajua kuwa Wenyeviti wa Kamati za Bunge au Mawaziri wa Serikali hawaandiki hotuba zao wenyewe, bali WANAANDIKIWA na watumishi ambao wameajiriwa kwa kazi hiyo. Hata yeye mwenyewe kwa nafasi yake haandiki hotuba zake, bali wako wasaidizi katika ofisi yake wanaofanya kazi hizo. Inakuwaje nongwa kwa Mawaziri Kivuli au Kambi ya Upinzani Bungeni kuandikiwa hotuba? Huku Mawaziri wakiwa na lundo la wasaidizi kwa maana ya watumishi wa serikali na Kamati za Bunge zikiwa na Sekretarieti zenye watu hadi 8 wanaofanya kazi za kutafiti, kuchambua na kuandika taarifa zinazosomwa bungeni na Wenyeviti?

Tulifikiri kuwa Spika Ndugai alipaswa kujisikia vibaya kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, chini ya uongozi wake, kinyume na utamaduni na utaratibu wa bunge letu na mabunge ya Jumuiya ya Madola, imelazimika kujichangisha na kutumia fedha kutoka mifuko ya wabunge wake wenyewe kutafuta watu wa kuwafanyia kazi kwa maana ya utafiti, uchambuzi na kuandika hotuba, jambo ambalo lilipaswa kuwa sehemu ya wajibu wa Ofisi ya Bunge.

Tunaamini Spika Ndugai anaelewa kuwa utaratibu wa Bunge kuajiri na kuwalipa watumishi wanaosaidia shughuli za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni upo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge na Kanuni za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambazo zimesajiliwa Ofisi ya Bunge.

Anatambua kuwa utaratibu huo umekuwepo tangu mabunge yaliyopita chini ya Spika Samuel Sitta, Spika Anne Makinda na hata chini ya Spika Ndugai, Ofisi ya Bunge imekuwa ikiwajibika katika suala hilo, hadi alipogeuka kwa baada ya masuala yaliyotokea wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki.

Tunatumia nafasi hii kusema yafuatayo;

1. Tunalaani na kukemea vikali uvunjifu mkubwa wa Kanuni za Kudumu za Bunge unaoendelea kufanywa na Bunge letu chini ya Spika Ndugai.

2. Tunapinga na kulaani kwa nguvu zote uamuzi huo wa bunge kuzuia kusomwa kwa hotuba ya bajeti mbadala, kinyume na Kanuni za Bunge letu.

3. Tunatoa wito kwa Spika Ndugai kutambua unyeti wa mamlaka ya Mhimili wa Bunge, majukumu ya wabunge na Bunge lote kwa ujumla. Na kwamba kwa nafasi yake anao wajibu wa kuhakikisha mamlaka hayo hayadhalilishwi hata mara moja kwa uvunjifu wa kanuni, iwe kwa vitendo au kauli.

4. Ni kutokana na mwanya unaotolewa na ofisi yake kutosimamia kikamilifu mamlaka ya mhimili huo kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria na Kanuni zake, imesababisha hata watu wengine kuona ni kawaida kuweza kuchezea mhimili huo. Mathalani tukio la watu wasiokuwa wataalam wa chakula na lishe, bila kufuata utaratibu, wameweza kuingia hadi jikoni kwenye mghahawa wa Bunge na kushika chakula kilichopikwa tayari, kwa kisingizio cha kukagua uvuvi haramu. Uko wapi usalama wa bunge na wabunge wenyewe?

5. Kwa kutambua umuhimu wa hotuba ya bajeti ya Kambi ya Upinzani Bungeni ambayo ilisheheni masuala muhimu kuonesha namna ambavyo CHADEMA na Kambi ya Upinzani Bungeni ni mbadala wa Serikali ya CCM, na kwa kutambua kuwa wananchi wamenyimwa fursa adhimu ya kusikia namna ambavyo CHADEMA na UKAWA wangefanya kuwakwamua wananchi katika hali ngumu wanayopitia iwapo wangekuwa madarakani, Chama kimeamua kuwa kwa kutumia mfumo wa chama, kitasambaza hotuba hiyo kwa wananchi nchi nzima ili waone tofauti kubwa iliyopo katika ya CCM iliyoshindwa na upinzani unaokwenda kuchukua dola. Kwa hatua ya sasa hotuba hiyo inapatikana kwenye Website ya Chama; www.chadema.or.tz.

Imetolewa leo Alhamis, Juni 21, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Share Button