MTAZAMO WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19

 

  1. UTANGULIZI

Kwanza niwashukuru kwa kuitikia mwito wa kuzungumza nanyi ili kupitia kwenu tuweze pia kuzungumza na Watanzania. Pili, niwatakie Waislam na Watanzania kwa ujumla Eid Mubarack na kuwapongeza wote walioshiriki katika ibada ya kufunga kulingana na matakwa ya imani yao.

Pili, napenda kuwajulisha Watanzania kuwa siku ya jumatatu tarehe 18 Juni, 2018 Kambi Rasmi ya Upinzani itawasilisha Hotuba Bajeti Mbadala kwa mwaka wa fedha 2018/2019

Tatu, Bajeti yetu mbadala itakuwa ni Bajeti ya ukuaji shirikishi wa uchumi kama tutakavyofafanua.

Hivyo basi mtazamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ni kama ifuatavyo;

  1. BAJETI YA SERIKALI NI HEWA

 Jambo la kwanza ambalo tungependa muwajulishe watanzania ni kwamba; tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani, imekuwa ikiwasilisha BAJETI HEWA Bungeni.

Nitatoa sababu za Bajeti Hewa:-

Sababu ya kwanza ya Bajeti kuwa hewa: ni kuweka makisio makubwa ya makusanyo ya fedha; na kushindwa kukusanya kiasi hicho. Kile kiasi kilichoshindikana kukusanya kinakuwa ni makusanyo hewa. Kwa mfano:-

  • Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 29.54 lakini iliweza kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote yaliyofikia shilingi trilioni 20.7 sawa na asilimia 70.1 ya lengo. Hii ina maana kwamba, asilimia takriban 30 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 8.83) ilikuwa ni makusanyo hewa.
  • Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 31.71 lakini iliweza kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 21.89 sawa na asilimia 69 ya lengo. Hii ina maana kwamba asilimia 31 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 9.82) ilikuwa ni hewa. Tazama Jedwali

Jedwali. Na.1. Makisio na Makusanyo halisi ya Mapato ya Serikali kwa miaka miwili.

MWAKA MAKISIO MAKUSANYO NAKISI
2016/17 Tril. 29.54 Tril. 20.7 (70%) Tril.8.83 (30%)
2017/18 Tril. 31.71 Tril.21.89 (69%) Tril.9.82 (31%)

Chanzo: Hotuba ya Waziri wa Fedha wakati wa kuwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18

 

Sababu ya pili ya Bajeti kuwa hewa; ni kutotekeleza kikamilifu bajeti iliyoidhinishwa na Bunge katika sekta mbalimbali. Nitatoa mifano katika wizara tatu zinazogusa maisha ya watu wengi moja kwa moja kwa miaka miwili (2016/17 na 2017/18):-

 

  1. Wizara ya Kilimo:-
  • Katika mwaka wa fedha 2016/17, Wizara ya Kilimo iliidhinishwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 100.527 lakini hadi Machi, 2017 zilitolewa shilingi bilioni 2.252 sawa na asilimia 2.22 ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge. Hii ina maana kwamba takribani asilimia 98 ya bajeti hiyo ilikuwa ni hewa ndio maana haikutekelezwa.
  • Katika mwaka wa fedha 2017/18; wizara hii iliidhinishiwa na Bunge fedha za maendeleo jumla ya shilingi bilioni 150.253 (150,253,000,000/-) lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2018; ni shilingi bilioni 16.5 tu (16,520,540,444/-) zilikuwa zimetolewa ikiwa ni sawa na asilimia 11 tu ya fedha za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa. Hii ina maana kwamba asilimia 89 ya bajeti ya maendeleo katika sekta ya kilimo ilikuwa ni hewa.

 

  1. Wizara ya Mifugo na Uvuvi:
  • Kwa mwaka wa fedha 2016/17 Wizara iliidhinishiwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 4 lakini zilizotolewa ni shilingi milioni 130 tu sawa na asilimia 3.25 ya bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa. Hii ina maana kwamba takribani asilimia 97 ya bajeti hiyo ilikuwa hewa ndio maana haikutekelezwa.
  • kwa mwaka wa fedha 2017/18 Wizara hii iliidhinishiwa na Bunge jumla ya shilingi bilioni 4 (4,000,000,000/=) kama fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya mifugo na uvuvi; lakini hadi kufikia mwezi machi, 2018 hakuna hata shilingi moja ambayo ilikuwa imepokelewa kutoka hazina kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta hizo. Hii ina maana pia kwamba asilimia 100 ya bajeti ya maendeleo katika sekta za mifugo na uvuvi ilikuwa ni hewa!

 

  • Wizara ya Maji
  • Kwa mwaka wa fedha 2016/17 Wizara iliidhinishiwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 913.836 lakini zilizotolewa zilikuwa ni bilioni shilingi 230.997 sawa na asilimia 25 ya fedha iliyoidhinishwa. Hii ina maana kwamba, asilimia 75 ya bajeti ya maendeleo katika sekta ya maji kwa mwaka huo haikutekelezwa, na kwa maana hiyo ni hewa.
  • Kwa mwaka wa fedha 2017/18, Wizara iliidhinishiwa shilingi bilioni 623.606 lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2018, fedha zilizokuwa zimetolewa ni shilingi bilioni 135.191 sawa na asilimia 22 ya fedha zilizoidhinishwa. Hii ina maana pia kwamba asilimia 78 ya bajeti ya maendeleo katika sekta ya maji haikutekelezwa. Tazama majedwali:

Jedwali Na. 2. Utekelezaji wa Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17

WIZARA BAJETI ILIYOIDHINISHWA FEDHA HALISI ILIYOTOLEWA %YA FEDHA ILIYOTOLEWA
KILIMO Bil.100.527 Bil. 2.252 2.22
MIFUGO+UVUVI Bil. 4 Mil. 130 3.25
MAJI Bil.913 Bil. 230.997 25

Jedwali Na. 3 Utekelezaji wa Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18

WIZARA BAJETI ILIYOIDHINISHWA FEDHA HALISI ILIYOTOLEWA % YA FEDHA ILIYOTOLEWA
KILIMO Bil. 150.253 Bil. 16.5 11
MIFUGO+UVUVI Bil.4 0 0
MAJI Bil.623 Bil 135.191 22

Chanzo: Randama za Wizara husika kwa mwaka 20116/17 na 2017/18

 

Sababu ya tatu inayoifanya Bajeti ya Serikali kuwa Hewa ni Utovu wa Nidhamu ya Matumizi ya Fedha kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 na Sheria ya Fedha.

Kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 41(1) ni kwamba; Ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutekeleza majukumu ya Serikali “Serikali itatakiwa kuwasilisha Bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa”. Aidha, utaratibu huu unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma wa mwaka 2001( Public Finacne Act, 2001)ambapo kifungu cha 18 (3) na (4) kinaitaka Serikali kuleta Bungeni bajeti ya nyongeza     (mini-budget) kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.

Utaratibu huo wa kisheria umekuwa ukivunjwa na Serikali kwa kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge jambo ambalo linaua dhana ya madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali; lakini pia kunatoa mwanya uwa wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Ikiwa matumizi yanafanyika nje ya bajeti; bajeti ya namna hiyo inakuwa hewa kwa kuwa haina Baraka za Bunge.

Ipo mifano mingi ya mtumizi ya Serikali yaliyofanywa nje ya Bajeti iliyodhinishwa na Bunge. Mifano hiyo ni pamoja na:-

  • Ujenzi wa Ukuta kwenye machimbo ya Tanzanite – Mirerani
  • Ujenzi wa Hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  • Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege – Chato
  • Kuhamishia Makao Makuu Dodoma bila bajeti ya kufanya hivyo

Aidha, zipo Wizara zilizopewa fedha zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali kwenye Kamati ya Bajeti ya Bunge kuhusu matumizi ya serikali kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 na mwelekeo hadi juni 2018 inaonyesha kwamba baadhi ya wizara zilipatiwa fedha zaidi ya bajeti iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kama ifuatavyo:-

 

  1. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, shilingi 4,616,070,000. Kiasi kilicholipwa hadi Machi 2018 ni shilingi 8,880,870,019 (257%)
  2. Tume ya Uchaguzi , bajeti iliyoidhinishwa na Bunge shilingi 2,470,031,000 . Kiasi kilicholipwa mpaka mwezi Machi 2018 ni shilingi 6.031,856,200 (326%)
  • Ofisi ya Rais (TAMISEMI), bajeti iliyidhinishwa na Bunge 8,212,296,000. Kiasi kilicholipwa mpaka mwezi Machi 2018 , shilingi 17,122,775.005 (278%)
  1. Wizara ya Mambo ya ndani. Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge shilingi 4,405,897,000. Kiasi kilicholipwa mpaka mwezi Machi 2018 ni shilingi 11,318,896,430 (343%)
  2. Ofisi ya Makamu wa Rais . Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge shilingi 2,879,167,000. Kiasi kilicholipwa mpaka mwezi Machi 2018 ni shilingi 5,811,478,145 (269%)

Matumizi yote haya ambayo hayakujumuishwa kwenye bajeti iliyoidhinishwa na Bunge yanaifanya Bajeti ya Serikali kuwa hewa kwa kuwa haizingatiwi katika kufanya matumizi

 

 

  1. MIRADI YA KISIASA YA SERIKALI YA KIPAUMBELE ISIYOKUWA NA MPANGO NA MKAKATI WA KIBIASHARA

Serikali ya awamu ya tano inatekeleza miradi ambayo sisi tunaona ipo kisiasa zaidi na hakuna mkakati wala mpango wa kibiashara ambao umewekwa wazi na Serikali hadi sasa.

Naomba kutoa ufafanuzi na uchambuzi kwenye miradi mitatu yaani Mradi wa Reli ya Standard Gauge (SGR), Ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme- MW 2,100 maarufu kama Stiegler’s Gorge na Kufufua Shirika la Ndege (ATCL) ambao Serikali imejikita kwenye mradi wa ununuzi wa Ndege;

 

  • Mradi wa Reli ya Standard Gauge kutoka Dar –es-Salaam hadi Mwanza ambao unatarajiwa kugharimu Trilioni 17.6 na unatarajiwa kukamilika 2021[1], ambapo kwa sasa umeanza kutekelezwa kuanzia Dar-es-Salaam- Morogoro KM 205 na Morogoro Makutupora KM 422[2].
  • Hakuna anayeweza kubisha au kupinga kuwa kama nchi tunahitaji reli ya kisasa kwa ajili ya kurahisisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
  • Serikali imejikita kwenye ujenzi wa miundombinu ya reli pekee na sio kufanya uchambuzi wa mradi mzima kuanzia utaratibu wa kuwa na mabehewa ya kisasa, mfumo wa uendeshaji ikiwemo kutoa mafunzo kwa madereva wataoendesha treni hizo, mafunzo kwa watoa huduma, mafunzo kwa watakaokuwa wanafanya shughuli za ukarabati wa miundombinu ya SGR.
  • Serikali haijaweka wazi na wala haina mpango wa kuendesha mradi wa SGR kibiashara zaidi ya kupiga porojo za Miundombinu pekee jambo ambalo linaonyesha kuwa tunaweza kuwa na mradi utakaolitia Taifa hasara.
  • Taarifa zinaonyesha kuwa SGR inajengwa kwa mikopo ya masharti ya kibiashara ambapo Taifa litalazimika kuanza kulipa madeni ya mradi huu kabla haujakamilika.

 

  • Stiegler’s Gorge

Mradi huu unategemewa kuzalisha MW 2100 kwa kutumia maji (Hydro Power Plant) katika Bonde la Mto Rufiji. Mpaka kukamilika kwa mradi kwa utafiti wa NORCONSULT wa mwaka 2006 mradi ulikisiwa kugharimu kiasi cha Tshs. Trillion 4 (Dola bilioni 2)[3] na kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha bilioni 700 kimetengwa na muda wa kumaliza mradi ni miezi 36 kuanzia Julai, 2018[4].

  • Bunge halijafahamishwa kuwa mradi utagharimu kiasi gani ingawa inakisiwa kuwa utagharimu Trilioni 7.
  • Itakumbukwa kuwa Serikali ilitumia takribani trilioni 1.2 kujenga bomba la gesi[5] kutoka Mtwara hadi Dar-es-Salaam[6].
  • Taarifa zinaonyesha kuwa kwa sasa Bomba la gesi hutumika kwa 6% pekee, kama Serikali itaweza kulifanya Bomba kutumika kwa 25% linawez kuzalisha MW 2000 takribani sawa na mradi wa Trilioni 7 wa Stigler’s Gorge. Bomba likitumika kwa 100% litaweza kuzalisha MW 10,000
  • Ni sababu zipi zinazoifanya serikali kutoendelea kuwekeza kwenye umeme wa gesi ambao miundombinu ipo tayari na kukimbilia kwenye mradi wa Stiegler’s Gorge ambao unagharimu Taifa trilioni 7?
  • Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kusitisha mradi huu na kuwekeza kiasi cha bilioni 700 zilizotengwa kwenye sekta za kiuchumi ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.

 

  • Kufufua Shirika la Ndege

Serikali imekua ikinunua Ndege kwa ajili ya kulifufua Shirika la Ndege la ATCL. Kwa mwaka huu Waziri wa Fedha amesema kuwa wamekamilisha kulipa gharama 30% ya gharama za ndege aina ya CS 300 na malipo ya 52% ya Boeng 787[7].

  • Mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kwa mujibu wa kitabu cha fedha za Maendeleo Volume IV Part A fungu 62 kasma 4294 ilitenga jumla ya shilingi Bilioni 500 fedha za ndani kwa ajili ya kununua ndege za abiria kwa ajili ya shirika la Ndege la ATCL.
  • Katika hali ya kushangaza tofauti na billion 500 zilizokuwa zimetengwa, Waziri wa Fedha akiwakilisha taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2016 na mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2016/17 alieleza Bunge kuwa serikali ilishasaini mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine 4 na malipo ya awali ya dola milioni 56.89 ambayo ni sawa na shilingi 126,125,130,000 yalifanyika. Je Bajeti hii iliidhinishwa na mamlaka gani?
  • Mfumo wa Manunuzi ya Ndege haujawekwa wazi hata baada ya Kambi kuhoji kwa miaka miwili mfululizo.
  • ATCL inategemea ruzuku ya Serikali na Waziri wa Fedha amekiri katika tathmini ya Bajeti ya mwaka uliopita moja ya changamoto ni utegemezi wa Mashirika ya Umma katika Bajeti ya Serikali[8].
  • Ili Ndege iweze kuwa na faida ni lazima itumie muda mwingi kusafiri na sio kuwa kwenye Viwanja vya Ndege. Kwa sasa nchini kuna Viwanja vine pekee ambavyo vina taa kwa ajili ya ndege kutua na kuruka usiku. Kwa hiyo ndege za Serikali haziwezi kutengeneza faida.
  • Hakuna mkakati wowote wa kibiashara wa kimataifa kwenye uboreshaji wa Shirika la Ndege. Hakuna mkakati wowote wa kuwa na Ndege za mizigo hasa mbogamboga na maua kwa ajili ya kusafirisha kwenda nje ya nchi.

 

  1. VIPAUMBELE VYA BAJETI MBADALA

Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itakua na vipaumbele katika sekta zafuatazo;

  • Elimu
  • Kilimo, Mifugo na Uvuvi (agrarian revolution)
  • Viwanda katika mnyororo wa thamani wa Kilimo (Agro- Processing Industries
  • Afya na Maji
  • Utawala Bora (Good Governance)

Pamoja na vipaumbele hivyo; naomba kuweka msisitizo kidogo katika Utawala Bora kwa kuwa Serikali hii imepuuza kabisa dhana ya utawala Bora jambo ambalo limeleta athari kubwa sana katika uchumi na hata mahusiano yetu kitaifa na kimataifa.

 

  • UCHUMI IMARA NI MATOKEO YA UTAWALA BORA

Ujenzi wa uchumi imara ni matokeo ya moja kwa moja na utawala bora katika nchi au ukuaji wa uchumi ni lazima uende sambamba na utawala bora. Lakini katika nchi nchi yetu kumekuwa na mambo yanayoifanya nchi yetu isiwe mahala salama kwa ajili ya uwekezaji. Matukio yafuatayo yanaathiri uwekezaji pamoja na utekelezaji wa Bajeti;

 

  • Kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya
  • Tishio la Watu wasiojulikana kuteka, kutesa na kupiga wananchi risasi.
  • Kuminywa kwa Vyombo vya Habari na uhuru wa kupata na kupokea habari kwa kutumia Sheria ya Huduma za Habari pamoja na Makosa ya Mtandao.
  • Kuboresha utawala wa sheria na sio utawala wa mtu binafsi

 

  1. MAPENDEKEZO YA MPANGO WA KUFUNGAMANISHA KILIMO NA MAENDELEO YA VIWANDA (AGRO ECONOMY)

 

Bajeti ya serikali 2018/2019 imeainisha sekta ya kilimo kama kipeumbele cha serikali lakini haijaonyesha ni kwa namna gani hasa inalenga kufanya Mapinduzi ya Kilimo (Agrarian Revolution) ili kuweza kusisimua sekta ya viwanda.

Sekta ya kilimo inachangia ajira kwa asilimia 66, pato la taifa kwa asilimia 30 lakini ukuaji wake unakuwa kidogo sana kwa wastani wa asilimia 3.7 na hivyo kuwa na mchango mdogo sana katika sekta ya viwanda. Kambi Rasmi ya Upinzani italenga kufanya kufanya yafuatayo;

 

  • Kuondoa kodi kwenye uwekezaji katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.Hii ni pamoja na kuondoa kodi kwenye viwanda vinavyotengeneza na kukarabati mashine, zana na pembejeo za kilimo, uvuvi na mifugo.
  • Uwepo wa umeme wa uhakika ili kuendesha shughuli za uzalishaji viwandani. Hivyo, itawekeza ipasavyo katika umeme wa gesi asilia.
  • Kushirikisha sekta binafsi kupitia mpango wa (PPP) ambapo serikali itawekeza kwenye mitaji ya uwekezaji kwa asilimia 40 na sekta binafsi itashirikishwa kwa asilimia 60.
  • Kuongeza idadi ya ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo na viwanda.
  • Kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja na pia Serikali itapanua wigo wa kodi.
  • Kusisimua sekta ya usafirishaji na mauzo nje ya nchi.

 

  1. MAENEO YA KIPAUMBELE KATIKA BAJETI MBADALA

 

  • Elimu
  • Kilimo, Mifugo na Uvuvi (agrarian revolution)
  • Viwanda katika mnyororo wa thamani wa Kilimo (Agro- Processing Industries
  • Afya na Maji

 

 

______________________

Freeman Aikaeli Mbowe

KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI

 

Share Button