TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

UHURU WA HABARI NI DEMOKRASIA

Wakati dunia ikiazimisha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani, ambayo huadhimishwa tarehe 3 Mei ya kila mwaka, huku zikiwepo nchi ambazo zimeendelea kunufaika na matokeo ya kuimarisha uhuru huo, taarifa zinaonesha kuwa Tanzania inazidi kuporomoka katika eneo hili hali inayotishia mstakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Kwa mujibu wa Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (SRF), ambalo hutoa hupima Uhuru wa Habari katika mataifa mbalimbali duniani, Tanzania imeshuka nafasi 10, kutoka nambari 83 mwaka 2017 hadi kuwa ya 93, mwaka huu.

Taarifa za mashirika mengine kama Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CJP) na Freedom House, pia zimeonesha kuwa Tanzania haifanyi vizuri katika suala la Uhuru wa Habari, kutokana na kuwepo kwa mazingira (ya kisiasa, kiuchumi na kisheria) yanayozidi kuminya uhuru huo.

Taarifa hizo ni sehemu ya uhalisia ambao Watanzania wenyewe wanaishi nao kwa kuuona au kuusikia. Sote tunajua kuwa ni hivi karibuni tu, Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana ya masuala ya habari, imepitisha kanuni za kusimamia maudhui ya habari za mitandao, ambazo zinaipatia Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) nguvu kubwa za kudhibiti uzalishaji, usambazaji wa habari, utoaji wa maoni na haki ya kupata taarifa katika blogs, majukwaa, redio na luninga za mitandaoni.

Mfano huo ni mwendelezo wa kuzorotesha mazingira ya Uhuru wa Habari nchini, chini ya utawala huu wa CCM tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, kwani kanuni hizo zinatonesha vidonda na kuongeza maumivu makali ambayo tayari yamesababishwa na ukali wa sheria kadhaa ambazo ni tishio kubwa la uhuru huo, zikiwemo Sheria za Makosa ya Mtandao na Sheria ya Takwimu.

Watanzania wanaadhimisha siku hii huku vyombo vya habari vikiwa bado vinaandamwa na jinamizi la adhabu kali kuliko wakati wowote ule baada ya mkoloni, ikiwemo kufutwa kwenye Orodha ya Msajili wa Magazeti (Gazeti la Mawio) kufungiwa muda mrefu (Mwanahalisi, Mseto, Raia Mwema, Tanzania Daima) au kutozwa kiwango kikubwa cha fedha (Azam Tv, ITV, EATV, Star Tv na Channel Ten).

Hayo yanaenda sambamba na kutishwa, kunyanyaswa, kufunguliwa kesi kwa waandishi na wadau wa habari kutokana na kutimiza majukumu yao na kutetea maslahi ya taifa (kesi ya Maxence Meelo na Mike Mushi wa JamiiForums na kupotea kwa Azory Gwanda).

Kutokana na kuendelea kuzorota kwa uhuru wa habari nchini ambayo ni dalili mbaya na tishio dhidi ya ustawi wetu kama taifa, CHADEMA tunatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kutafakari kwa kina hali hii, huku wakipinga na kukemea kwa nguvu zote juhudi za baadhi ya watu, hususan wenye mamlaka kujaribu kuifanya Tanzania ni sehemu ya ‘kilio cha samaki’, kwa sababu kuzuia uhuru wa habari ni kuminya sauti (kilio) za wananchi kuonesha hisia zao juu ya jambo lolote ikiwemo namna wanavyoongozwa au kutawaliwa.

CHADEMA kama taasisi ya kisiasa pekee ya kisiasa nchini iliyotia saini Tamko la Dar es Salaam la Uhuru wa Habari na Uwajibikaji, kwa kushirikiana na wadau wengine wote wenye nia njema, itaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea Uhuru wa Habari, vyombo vya habari na wanahabari, kwa sababu hauwezi kutenganisha Uhuru wa Habari na Demokrasia kama sehemu ya misingi muhimu ya maendeleo ya kweli kwa taifa na ustawi wa jamii.

Imetolewa Alhamis, Mei 3, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Share Button